Rotimi ahirisha ziara zake ikiwemo ya Kenya

Muhtasari

 

•Tunafanya kazi kwa bidii pamoja na washirika wetu  ili kukamilisha ratiba iliyoahirishwa  ambayo itatangazwa hivi karibuni

Venessa Mdee na Rotimi
Venessa Mdee na Rotimi
Image: Instagram

Rotimi ametangaza kuahirisha ziara zake zilizokuwa zimepangwa kufanyika mwaka huu kufuatia ongezeko la virusi vya Corona.

Kupitia ukurusa wake wa instagram, ametoa taarifa kwa mashabiki wake huku akiwaeleza kiini cha kuahirisha  ziara alizopanga kufanya hivi karibuni. 

kulingana naye ongezeko la virusi vya Corona, hasa  kirusi cha Omicron ambacho kinasemekana kuenea kwa kasi ndio sababu kuu yake kusitisha ziara zake. 

"Kwa sababu ya kuongezeka kwa visa vya covid... kikosi changu na mimi tumefanya uamuzi mgumu wa kuahirisha ziara." Rotimi alieleza 

Mpenzi huyo wa mwanamuziki mashuhuri kutoka nchi ya Tanzania, Vanessa Mdee, amewaeleza mashabiki wake  ambao  walikuwa tayari washanunua tiketi kwamba wasiwe na shaka kwani tiketi hizo zitasalia halali hadi wakati atakapopanga hafla nyingine ya muziki.

"Tunahisi ni bora kwa usalama wa mashabiki na wafanyakazi wangu. Tiketi zote zilizonunuliwa zitasalia kuwa halali kabisa na zitapatikana kutumika katika tarehe mpya.

Kwa mashabiki ambao wangependa kurejesha tiketi zao aliwahakikishia kuwa wasiwe na wasiwasi kwani pia hilo linawezekana.

"Ikiwa ungependa kurejesha  tiketi zako, hilo linawezekana pia. Tunafanya kazi kwa bidii pamoja na washirika wetu  ili kukamilisha ratiba iliyoahirishwa  ambayo itatangazwa hivi karibuni. Ninathamini upendo na msaada wenyu. Tafadhali kaa salama na nitakuona hivi karibuni"