Wasagaji na mabasha wapinga kauli ya Magoha

Muhtasari

• Watu wa jamii ya wapenzi wa jinsia moja au ukipenda mashoga wamepinga vikali hoja ya waziri wa elimu George Magoha kutaka wanafunzi mashoga kusomea shule za kutwa.

• Wanachama wa jamii hiyo waliandamana siku ya Alhamisi kufuatia kauli ya Waziri wa Elimu George Magoha wakisema kwamba ni ya kibaguzi.

Makena Njeri
Image: Studio

Watu wa jamii ya wapenzi wa jinsia moja au ukipenda mashoga wamepinga vikali hoja ya waziri wa elimu George Magoha kutaka wanafunzi mashoga kusomea shule za kutwa.

Wanachama wa jamii hiyo waliandamana siku ya Alhamisi kufuatia kauli ya Waziri wa Elimu George Magoha wakisema kwamba ni ya kibaguzi.

Wanachama hao wakiongozwa na Makena Njeri,  waliwasilisha mapendekezo yao kwa wizara ya elimu.

Walipinga uamuzi wa waziri wa Elimu George Magoha  kuwataka watoto wenye tabia za ushoga kusoma shule za kutwa  ambazo ziko karibu na maboma yao.

Alisema ombi lao kwa wizara ya elimu ni kuhakikisha hawajakubali pendekezo la waziri wa elimu kuwa wanafunzi wa wenye hulka ya ushoga wasikubaliwe shule za bweni.

"Leo tulikuwa na dhamira moja. kuandamana barabarani hadi  wizara ya elimu kukabidhi ombi letu kwa CS. Haya yanajiri baada ya kauli za kibaguzi zilizotolewa na Waziri wa Elimu  mapema mwezi huu, kuwa watoto mashoga hawafai kuruhusiwa katika shule za bweni, huu ni upuuzi ulioje." alisema Makena Njeri.

Alieleza dhamira ya mandamano yao ilikuwa kuwakumbusha viongozi kuwa wanapaswa kuwalinda watoto wote  kupata haki  ya kupata elimu.

"Maandamano yetu ya leo yalikuwa ni kuwakumbusha viongozi kuwa wanapaswa kuwalinda watoto wote, wako na  haki ya kupata elimu popote pale wanapotaka bila kujali utambulisho wao wa kijinsia au mwelekeo wao wa kimapenzi. Watoto wa Jamhuri ya Kenya wana haki na hawatabaguliwa na serikali ile ambayo inapaswa kuwalinda."