"Niko na moto!" Mwanamuziki Justina Syokau akiri anatamani kuolewa tena

Muhtasari

•Justina amesema kuwa kwa sasa anajiskia kama kwamba hisia zake za mapenzi zimerejea na kudai angependa kupata mchumba.

•Amekiri kwamba amekuwa bila mchumba kwa kipindi cha miaka nane tangu alipotengana na mumewe.

Image: INSTAGRAM// JUSTINA SYOKAU

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Justina Syokua almaarufu kama 'Twendi Twendi' amesema kuwa sasa yuko tayari kuolewa tena.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mwanamuziki huyo alikiri kwamba amekuwa bila mchumba kwa kipindi cha miaka nane tangu alipotengana na mumewe.

Justina amesema kuwa kwa sasa anajiskia kama kwamba hisia zake za mapenzi zimerejea na kudai angependa kupata mchumba.

"Mwaka wa 2020 ndio nilisema najiskia kama hisia zangu zimerejea. Sasa naweza kuolewa. Bibilia inasema wakati uko na moto olewa, usije ukatenda dhambi. Mimi siwezi taka kutenda dhambi. Niko na moto, moto imerudi. Mungu ndio aliruhusu hii yote. Kama hangetuumba na viungo hivi hatungekuwa na shida" Justina alisema.

Mwanamuziki huyo alisema alianza kugundua kwamba anahitaji mchumba baada ya janga la Corona kushambulia ulimwengu.

Amesema wakati nchi ilifungwa alipatwa na upweke akiwa nyumbani kwake na mwili wake ukaanza kusisimka kuashiria kuwa anahitaji mchumba.

"Nimekuwa single miaka nane. Tangu nilipotoka kwa mume wangu sijakuwa katika mahusiano. Kwanza niliangazia kulea. Kitu ambacho kimefanya nigundue niko single ni kuja kwa Covid. Katika kipindi hiki cha Covid nimegundua kumbe niko. Nilianza kuhisi mwili imeamka. Nilikuwa nakaa kwa nyumba hakuna mahali kwa kwenda kuimba. Nilikuwa nakula tu hakuna kitu kingine. Mwili ilianza kuamka nikagundua kumbe Justina yuko. Hapo ndipo nilianza kufikiria kuhusu ndoa" Alisema Justina.

Justina alikiri kwamba hapo awali hakuwahi kufikiria angetamani kuolewa tena baada ya ndoa yake ya kwanza kugonga mwamba.

Alieleza kwamba katika kipindi hicho cha miaka nane ambacho hajakuwa na mchumba amekuwa akiangazia ulezi wa mtoto wake na akiomba Mungu amsaidie kupona kutokana na kuvunjwa moyo.