"Nimeongeza kilo 18" King Kaka azungumzia maendeleo ya afya yake baada ya kuugua kipindi kirefu

Muhtasari

•King Kaka alifichua kwamba kwa sasa yuko imara kiafya na tayari ameongeza takriban kilo 18 baada ya kuwa amepoteza zaidi ya kilo 33 wakati alipokuwa anaugua.

•Alisema safari yake ya kupata afueni iling'oa nanga mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita baada ya kuwa anaugua kwa kipindi kirefu.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amezungumza kuhusu hali yake ya afya kwa sasa baada ya kuwa anaugua kwa zaidi ya miezi mitatu  mwaka jana.

Akiwa kwenye mahojiano na Mwafreeka katika kipindi cha 'Iko nini', King Kaka alifichua kwamba kwa sasa yuko imara kiafya na tayari ameongeza takriban kilo 18 baada ya kuwa amepoteza zaidi ya kilo 33 wakati alipokuwa anaugua.

Rapa huyo aliweka wazi kuwa hamu yake ya chakula na hisia ya ladha tayari zimerejea kikamilifu na kwa sasa anaweza kula chakula vizuri.

"Hiyo iliisha. Niko na hisia ya ladha, nakula. Kuna wakati ilifika nikaanza kula. Nilipatiwa madawa ya kunisaidia kurejesha hamu ya chakula. Saa hii niko na kilo 78, nilikuwa nimepunguza uzito wa mwili hadi kilo 60. Saa hii nimeongeza 18. Hata daktari aliniambia ameshangaa jinsi  nilivyoongeza haraka" King Kaka alisema.

Kaka alisema wakati alipokuwa anaugua alikuwa amepoteza hisia yake ya ladha pamoja na hamu ya chakula, hali ambayo ilimfanya apoteze uzito mkubwa wa mwili.

Alisema wakati huo harufu ya chakula pekee ingeweza kumuathiri kiasi kwamba angeanza kutapika punde tu baada ya kukinusa.

"Sikuwa nakula. Nilikaa takriban wiki moja kama sijakula. Nilikuwa nakunywa maji tu. Nikiona chakula ningeanza kutapika tu. Sikuwa na ladha, siku moja niliamka nikajaribu kunywa uji. Lunch nilikula vijiko mbili. Daktari alisema niachwe nimejaribu. Mama angeleta chakula hospitalini kila siku.Nilianza kunywa supu polepole" Alisema.

Mwanamuziki huyo alisema safari yake ya kupata afueni iling'oa nanga mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita baada ya kuwa anaugua kwa kipindi kirefu.

King Kaka aliweka wazi kwamba hana kinyongo chochote dhidi ya daktari aliyempima vibaya na kumpa madawa yasiyofaa ambayo yalisababisha ugonjwa wake. Alisema tayari amemsamehe ila akamsihi awe mwangalifu zaidi.