Hamisa Mobetto azungumzia madai ya mahusiano ya kimapenzi kati yake na Rick Ross

Muhtasari

•Wawili hao wamedaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi kufuatia matendo yao ya kutiliwa shaka kwenye mitandao ya kijamii.

•Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alisisitiza kwamba kwa sasa anaangazia kukuza nembo yake na kujipatia utajiri zaidi.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamuziki na mwigizaji mashuhuri kutoka Tanzania Hamisa Mobetto amepuuzilia mbali uwepo wa mahusiano ya kimapenzi kati yake na rapa wa Marekani William Leonard Roberts II almaarufu kama Rick Ross.

Wawili hao wamedaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi kufuatia matendo yao ya kutiliwa shaka kwenye mitandao ya kijamii.

Alipokuwa kwenye mahojiano na NTV, mlimbwende huyo aliweka wazi kwamba Rick Ross ni rafiki wake wa karibu na mshirika wake wa kibiashara.

“Sisi ni kama familia kubwa na tumefanya vitu vingi pamoja ambavyo nitakuwa navizindua hivi karibuni’’, Mobetto alisema.

Mobetto alizungumza wakati wa ziara yake nchini Kenya ambapo anahusika na kazi za hisani katika mtaa wa Kayole,  Nairobi.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alisisitiza kwamba kwa sasa anaangazia kukuza nembo yake na kujipatia utajiri zaidi.

Mobetto pia alifichua kwamba amefanya kolabo ya muziki na Bien wa Sauti Sol pamoja na Otile Brown ambazo zitakuwa zinaachiliwa hivi karibuni.

Takriban miezi miwili iliyopita wasanii hao walizua gumzo kubwa mitandaoni baada ya kuonekana wakijiburudisha pamoja katika maeneo mbalimbali ya burudani jijini Dubai.

Matendo ya Mobetto na Rick Ross waliacha wafuasi wao na maswali chungu nzima huku wengi wakiamini kuna kitu kinachoendelea kati yao.