Profesa Hamo adokeza kuhusu mipango yake ya kujiunga na siasa

Muhtasari

•Kilichoibua hisia zaidi kwamba huenda anamezea kiti kimoja cha ubunge cha eneo hilo ni kuwa alijitambulisha kama Mheshimiwa  Prof Hamo.

Profesa Hamo
Profesa Hamo
Image: Instagram

Mchekeshaji mashuhuri nchini Herman Kago almaarufu kama Profesa Hamo amedokeza kuwa huenda anajiandaa kujitosa kwenye siasa za mwaka huu ambazo zimeonekana kuvutia wasanii wengi.

Siku ya Jumanne mtangazaji huyo wa zamani alipakia bango la kampeni kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akiwaomba wakazi wa eneo bunge la Nakuru  Mashariki kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kama wapiga kura.

Kilichoibua hisia zaidi kwamba huenda anamezea kiti kimoja cha ubunge cha eneo hilo ni kuwa alijitambulisha kama Mheshimiwa  Prof Hamo.

"Nakuru East Tuchukue Kura , Mh Prof Hamo, Vijana ni wakati wetu!!" Bango ambalo Hamo alipakia lilisoma.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha tangazo hilo na ujumbe "Hatuwezi kulalamika tena, tuchukue usukani wa  hatima yetu"

Mamia ya wanamitandao wameendelea kutoa hisia zao kufuatia hatua ya mume huyo wa wake wawili.

Sammy Kamaa: Unaweza kuwa mchekeshaji mzuri bungeni.

Irungu Faith: Mnatuchekesha kidogo, mnapata following mnafikiria mnaweza kuwa viongozi?

Daniel Bundi: Vile naona bunge hivi karibuni itakuwa kama jukwaa la kimataifa la matumbuizo.

Esther Baibs: Hesabu kura yangu kwenye kitabu chako

Edward Mung'au: Nakutakia kila lakheri. Kweli hatuwezi kulalamika milele.

Iwapo Hamo hafanyi mzaha na tangazo hilo basi atakuwa anajiunga na orodha kubwa inayoendelea kukua ya wasanii abao wamejitosa kwenye siasa.