Milly Chebby afunguka kuhusu wakati alitaka kugura ndoa yake na Terence Creative

Muhtasari

•Milly alisema katika miaka yao ya kwanza kwanza ya ndoa  alikusudia kumtema Terence kwa kuwa mchekeshaji huyo alikosa maoni na hakujali sana kuhusu maisha.

•Alieleza kwamba hakuwahi kumlaumu Terence kwa mtazamo huo wake wa maisha usio wa kupendeza ila alilaumu malezi yake

Image: INSTAGRAM// TERENCE CREATIVE

Mwanavlogu mashuhuri Millicent Chebet almaarufu kama Milly Chebby amekiri kwamba aliwahi kufikiria kugura ndoa yake na mchekeshaji Lawrence Macharia almaarufu kama Terence Creative.

Akiwa  kwenye mazungumzo na mumewe kwenye YouTube channel yake, Milly alisema katika miaka yao ya kwanza kwanza ya ndoa  alikusudia kumtema Terence kwa kuwa mchekeshaji huyo alikosa maoni na hakujali sana kuhusu maisha.

Milly alisema alikuja kutulia baada ya mumewe kukubali kubadilika huku akiweka wazi kwamba kwa sasa hajuti kuwa mke wake.

"Kwa sasa sina majuto ya kukuchumbia (Terence). Hapo awali, ndio. Kuna miaka ambayo nilitaka kuenda. Hukuwa mtu mwenye ndoto, hukujali kuhusu maisha. Ungeniambia kwamba ulilelewa kwa shida na hujalishwi na pesa. Ningekushinikiza uwe na ndoto" Milly alimwambia mumewe.

Milly hata hivyo alieleza kwamba hakuwahi kumlaumu Terence kwa mtazamo huo wake wa maisha usio wa kupendeza ila alilaumu malezi yake.

Alisema alielewa mazingira ambayo mumewe alilelewa yalichangia sana katika kujenga tabia hiyo maishani mwake.

"Shida haikuwa wewe. Nilifahamu kwamba ukionyeshwa njia nzuri ama ukae na watu ambao wanafanya mambo mazuri  kama wanaokaa na familia na wanakusudia kuwa wazazi ungeweza kubadilika. Nashukuru Mungu kuona kwamba maisha niliyoona wakati huo ndiyo tunaishi sasa" Milly alimwambia Terence.

Wawili hao wamekuwa kwenye ndoa kwa kipindi cha takriban mwongo mmoja na wamebarikiwa na mtoto mmoja pamoja.