"Dawa ya baloon ni sindano!" Sandra Dacha ataja sifa za mpenziwe Akuku Danger zilizomvutia zaidi

Muhtasari

•Dacha alimtambulisha mchekeshaji huyo ambaye amekuwa akiugua kwa wiki kadhaa kama mpenzi wake.

•Uvumi umekuwepo miongoni mwa mashabiki wao kwamba wawili hao ni wapenzi kutokana na ukaribu mkubwa walio nao.

Sandra Dacha almaarufu kama Silprosa na mpenzi wake Akuku Danger
Sandra Dacha almaarufu kama Silprosa na mpenzi wake Akuku Danger
Image: INSTAGRAM// SANDRA DACHA

Hivi majuzi mwigizaji mashuhuri nchini Sandra Dacha anayefahamika zaidi kama Silprosa kutokana na kipindi cha Auntie Boss aliweka bayana mahusiano yake ya kimapenzi na mchekeshaji Akuku Danger.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Dacha alimtambulisha mchekeshaji huyo ambaye amekuwa akiugua kwa wiki kadhaa kama mpenzi wake.

Dacha aliweka wazi kwamba mahusiano yao yaamekuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa huku akimtaja mchekeshaji huyo kama mpenzi wa chaguo lake.

"Tumekuwa kwenye mahusiano mwaka mmoja. Dawa ya baloon ni sindano. Yeye ni chaguo langu," Dacha alisema.

Mwigizaji huyo ambaye kwa kawaida hujitambulisha kama 'The biggest Machine' kutokana na ukubwa wa mwili wake alitaja moyo wa Akuku na tabasamu lake kama baadhi ya sifa zilizomvutia zaidi kwake.

"Ako na moyo wa dhahabu. Tena tabasamu lake, Mungu wangu!!Ushawahi ona akicheka?? Ni mtu mpoa sana" Dacha alisema.

Ufichuzi huu unajiri kama uthibitisho wa uvumi ambao umekuwepo miongoni mwa mashabiki wao kwamba wawili hao ni wapenzi kutokana na ukaribu mkubwa walio nao.

Dacha pia alihakikishia mashabiki kwamba kwa sasa mpenzi wake amepona ila akatoa wito kwa mchango zaidi ili kuweza kukamilisha bili ya hospitali.