"Nilipatwa na mshangao!" Babake Diamond azungumzia mzozo wake na mzazi mwenza, Mama Dangote

Muhtasari

•Mzee Abdul alisema hakutarajia mke huyo wake wa zamani angewahi kumtenga na familia na kusisitiza hakukuwa na mpangilio wowote.

•Aliendelea kufichua kwamba anapanga kufunga ndoa nyingine hivi karibuni maraa baada ya mipangilio muhimu kukamilika.

Mzee Abdul azungumzia ugomvi wake na Mama Dangote
Mzee Abdul azungumzia ugomvi wake na Mama Dangote
Image: HISANI

Baba ya mwanamuziki Diamond Platnumz, Mzee Abdul Juma amekiri kwamba alipatwa na mshangao mkubwa baada ya mamake msanii huyo Bi Sanura Kassim almaarufu kama Mama Dangote kumkana kama mzazi mwenza.

Akiwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Mzee Abdul alisema hakutarajia mke huyo wake wa zamani angewahi kumtenga na familia na kusisitiza hakukuwa na mpangilio wowote.

Abdul hata hivyo amesema tayari ameyasahau yaliyotokea kati yake na mzazi mwenzake na anaendelea vyema na maisha yake.

"Kuhusu stori ambayo ilitokea na Sanura, mzazi mwenzangu kunitenga  bila mpangilio na kujielewa, nilipatwa na mshangao. Hata hivyo nimesahau, maisha yanaendelea kusema kweli. Bado maisha yanaendelea, namshukuru Mwenyezi Mungu" Mzee Abdul alisema.

Bw Abdul alifichua kwamba kufikia sasa amewahi kuwa katika ndoa tatu maishani. Alisema ndoa na Mama Dangote ndiyo ilikuwa yake ya mwisho.

Aliendelea kufichua kwamba anapanga kufunga ndoa nyingine hivi karibuni maraa baada ya mipangilio muhimu kukamilika.

"Nilipata mtu wa dini tofauti, ni mtu tumekaa naye kwa muda. Sasa hivi tuko katika makubaliano. Ndoa itakuwa haina sherehe kwa sababu tayari nimefanya ndoa tatu haina haja ya sherehe. Itakuwa tu ya kiundani na watu wangu wa karibu, itakuwa kumchukua, kumbadilisha dini na kumpa jina basi" Alifichua Mzee Abdul.

Takriban mwaka mmoja uliopita Mama Dangote alishangaza wengi baada ya kudai kuwa Mzee Abdul sio baba mzazi wa Diamond Platnumz  kando na ilivyoaminika ikiaminika kwa miaka mingi.

Kwa sasa Mama Dangote ako kwenye mahusiano na mwanamume anayetambulika kama Uncle Shamte.