'Ingekuwa kukosa heshima akimpost mpenziwe mpya,' Mulamwah aeleza mbona alichukua akaunti za Muthoni

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alidai kuwa mama huyo wa mtoto wake mmoja alizitumia akaunti hizo vibaya ndiposa zikachukuliwa.

•Mulamwah alisema hakuridhishwa na mambo ambayo mpenzi huyo wa zamani alikuwa anachapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amekiri kuwa ni kweli timu yake ilichukua akaunti za mitandao ya kijamii za aliyekuwa mpenzi wake mwigizaji Carol Muthoni.

Akiwa kwenye mahojiano na Sauti TV, mchekeshaji huyo alidai kuwa mama huyo wa mtoto wake mmoja alizitumia akaunti hizo vibaya ndiposa zikachukuliwa.

Mulamwah alisema kuwa timu yake ilikuwa na haki ya kuchukua akaunti za Muthoni kwa kuwa wao ndio waliziunda na kumsaidia kuzisimamia.

"Niko na kampuni ya Mulamwah Entertainment. Wao ndio hufungua akaunti zote. Huwa wanazisimamia na kusaidia mtu kuonekana mzuri. Hivo ndivyo huwa wanatengeneza chapa yako wakitarajia kuwa siku ambayo utaanza kuingiza pesa pia zitaingia kwa kampuni. Hata kama tulikuwa tunachumbiana, yeye bado ni msanii. Ikifika wakati ambapo unataka kuenda, sisi hatutapata mapato ya uwekezaji, itakuwa tumeunda akaunti za nini.

"Ni kutumia vibaya ambako kulifanya akaunti zichukuliwe. Akaunti hizo zilikuwa zinatumiwa vibaya kwa kuwa, sisi tulitengana vizuri, tukachapisha na ikaisha. Keshoye aliamkia Youtube ati 'meet my mubaba', 'meet my nani'.. anafikiri ni kuwa mjanja ila sivyo. Ata asiponiongelea na anaongea kuhusu mubaba, anaambia mamake kuwa amesonga mbele na maisha yake, kila kitu kinanirejelea. Yeye ndiye alifanya kila kit kuwa kikubwa," Mulamwah alisema.

Mulamwah alisema hakuridhishwa na mambo ambayo mpenzi huyo wa zamani alikuwa anachapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Alisema kuwa kampuni yake iliafikia hatua ya kushikilia akaunti za Muthoni kwa muda baada ya kuona kuwa alikuwa anazitumia kufanya kesi yao ya kutengana kuwa mlima mkubwa.

"Sisi hatukuwa na noma yoyote, ni vile tu zilikuwa zinatumiwa vibaya wakati huo. Tulikuwa tunaamkia kwa blogs ati nani amesema haya, na tunapigwa vita na mtu ambaye tumetengeneza.. Hatuna ugomvi wowote, ni vile tu labda hatukuingiana kibiashara. Hatukuwa  tunataka kukaa na akaunti zake, ni vile tu aliamua kufungua zingine tukasema aendelee. Tena ingekuwa ukosefu wa heshima kuona anapakia mpenzi wake kwa akaunti uliunda. Huo ni upuzi bana. Biashara huwa haiendi hivo," Alisema.

Mchekeshaji huyo alidai kuwa alimsaidia mzazi huyo mwenzake kupata kazi za kufanya matangazo kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa sasa Muthoni anatumia akaunti mpya ambazo aliunda mwenyewe wiki chache zilizopita baada ya kupokonywa umiliki wa zile za awali.