BASATA yawapiga WCB Wasafi kifaa butu kichwani

Muhtasari

• Baraza la sanaa Tanzania (BASATA) limewatema wasanii wote kutoka WCB Wasafi nje ya orodha ya kuwania tuzo za Tanzania Music Awards.

Image: WASAFI

Wikendi iliyopita kumekuwa na maneno mengi mitandaoni yenye hisia kinzani baada ya baraza la sanaa Tanzania, BASATA kutoa orodha ya wasanii watakaowania tuzo katika vitengo mbalimbali.

Minong’ono hiyo imetokana na kwamba katika orodha hiyo, hakuna msanii hata mmoja kutoka rekodi lebo ya WCB Wasafi ambaye ameorodheshwa.

Kulingana na mabango ya BASATA ya orodha hiyo ambayo wameipakia kwenye instagram yao, wasanii wengi tu tena nguli kutoka nje ya Wasafi wametajwa mule lakini wale wenye uswahiba na Wasafi, wakiwemo Rayvanny na msanii wake MacVoice kutoka Next Level Music wamezimiwa taa za mchana.

Wasanii kama vile Alikiba, Harmonize, Nandy, Juma Jux, Marioo ni baadhi ya majina tajika ambyo yameonekana kwenye orodha ya kuwania Tanzania Music Awards katika vipengele tofauti tofauti.

Kukosekana kwa wasanii wa Wasafi kunatajwa kutokana na msanii Diamond Platnumz kutofautiana wazi na BASATA kwa kusema kwamba hajawahi nufaika na marupurupu yanayotolewa na baraza hilo kwa wasanii.

Diamond pia alilalamikia hatua ya muigizaji Steven Nyerere kuteuliwa kuwa msemaji na mratibu wa mipango wa wasanii kwa kile alikitaja kuwa hakufaa kwa sababu yeye si msanii wa bongo fleva.

Bila shaka hii ni vita kati ya rekodi lebo ya Wasafi na baraza la Sanaa ambapo kwa mara ya kwanza katika tukio hili ambalo si la kawaida, wasanii wote wa Wasafi hawatawania tuzo yoyote katika Tanzania Music Awards.