Rayvanny awatambua Bahati na Diana Marua kama wanandoa bora Afrika Mashariki

Muhtasari

•Rayvanny amejitokeza kuwa mmoja wa mashabiki wa wazazi hao wa binti mmoja na kijana mmoja huku akiwataja kama wanandoa bora zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY, BAHATI

Mwamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati na mkewe Diana Marua ni wanandoa ambao wameishi kusherehekeana hadharani tangu walipojitosa kwenye mahusiano zaidi ya miaka sita iliyopita.

Wawili hao wamekuwa wakishangiliwa na wengi kwa mafanikio yao katika ndoa na vilevile kukosolewa na kikundi kikubwa cha wanamitandao hasa kutokana na tofauti  zao za kiumri.

Staa wa Bongo Rayvanny amejitokeza kuwa mmoja wa mashabiki wa wazazi hao wa binti mmoja na kijana mmoja huku akiwataja kama wanandoa bora zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki.

"Best East African Couple (Wanandoa Bora Afrika Mashariki)" Rayvanny aliandika chini ya chapisho moja  la Diana kwenye Instagram.

Katika chapisho hilo la Jumapili, Diana na Bahati walionekana wakisakata densi nyumbani kwao huku wimbo wa Rayvanny 'Kiuno' ukicheza.

"Yooo!!! Nilifunga ndoa na rafiki wangu wa dhati Bahati. Tuteremke chini mpenzi," Diana aliandika chini ya video aliyopakia.

Rayvanny kwa upande wake kwa sasa anaaminika kuwa anachumbia binti ya mwigizaji Kajala Masaja, Bi Paula Kajala. Ana mtoto mmoja na mpenzi wake wa zamani Fahyma almaarufu Fayvanny.