"Daddy tuonyeshe njia" Akothee amsihi Ezekiel Mutua kutajirisha wanamuziki wa Kenya

Muhtasari

•Akothee amemwomba Mkurugenzi Mtendaji huyo wa zamani wa KFCB kuwasaidia wasanii kuweza kuvuna mazao ya kazi zao.

•Mutua alisema lengo lake ni kuona wanamuziki wa Kenya wametajirika, wameheshimika na kupata ushawishi mkubwa. 

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu kama Akothee ameikaribisha ahadi ya bosi mpya wa MCSK, Ezekiel Mutua kuwa atawakwamua wanamuziki wa Kenya kutoka  kwenye ufukara.

Akothee amemwomba Mkurugenzi Mtendaji huyo wa zamani wa KFCB kuwasaidia wasanii kuweza kuvuna mazao ya kazi zao.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 alikuwa anaunga mkono kauli ya Mutua kuwa "Inauma sana kuona wanamuziki wakiandaa harambee wanapougua."

"Daddy tuonyeshe njia, tumechoka kuonewa," Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Katika taarifa yake ya hivi majuzi, Mutua alisema lengo lake ni kuona wanamuziki wa Kenya wametajirika, wameheshimika na kupata ushawishi mkubwa. 

Alisema haridhishwi na hali ya sasa ya wanamuziki wa Kenya huku akiahidi kutia juhudi kuhakikisha kwamba wamesaidika.