"Natamani nicheze harusi yako kabla sijakata kauli," Mama Dangote amlilia mwanawe Diamond Platnumz

Muhtasari

•Diamond anamtaka Diamond amvishe pete mchumba wake punde baada ya mwezi mtakatifu wa Ramadhan kuisha.

•Hapo awali Mama Dangote alitangaza kwamba ameridhishwa na mpenzi mpya wa mwanawe huku akimwomba atulie naye sasa.

Diamond na mamake Mama Dangote
Diamond na mamake Mama Dangote
Image: INSTAGRAM// MAMA DANGOTE

Bi Sanura Kassim almaarufu kama Mama Dangote ameendelea kumpa shinikizo mwanawe Diamond Platnumz afunge ndoa hivi karibuni.

Mama huyo wa watoto watatu anamtaka Diamond amvishe pete mchumba wake punde baada ya mwezi mtakatifu wa Ramadhan kuisha.

Kulingana na Mama Dangote, Diamond tayari ashampata mwanadada anayekusudia kumfanya mke na kilichosalia  ni harusi rasmi tu.

"Mwanangu Naseeb Diamond Platnumz🦁. Nadhani unajua kilio changu cha kila siku kwako, Natamani nicheze harusi yako kabla sijakata kauli. Ushampata mwenza ndio umuoe Ramadhan ikiisha nawe uwe ndani ya ndoa Mwanangu," Mama Dangote alimwambia mwanawe kupitia mtandao wa Instagram.

Haya yanajiri huku tetesi za Diamond kuoa mwanamke mrembo kutoka Zanzibar zikiendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Hapo awali Mama Dangote alitangaza kwamba ameridhishwa na mpenzi mpya wa mwanawe huku akimwomba atulie naye sasa.

"Nashindwa kuelezea furaha yangu mwanangu, Naseeb Diamond Platnumz🦁, hapa sasa umepata mwenza. Utulie babangu uoe," Mama Dangote alisema.

Dadake Diamond alifichua kwamba tayari barua ya kupeleka kwa mashemeji wao ipo tayari na kilichosalia ni harusi tu.