Mulamwah amshtumu Sonnie kwa kutokuwa mwaminifu huku akifunguka sababu za kumtema

Muhtasari

•Mulamwah alidai kwamba mama huyo wa binti yake alikuwa na mahusiano na jamaa mwingine kwa zaidi ya mwaka mmoja.

•Amedai kwamba alimtema mwigizaji huyo baada ya kuzaliwa kwa binti yao kwani alishindwa kabisa kusahau ya kale.

Image: INSTAGRAM/CAROL SONNIE

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah sasa anadai aliyekuwa mpenzi wake Caroline Muthoni hakuwa mwaminifu kwake.

Alipokuwa anashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram, Mulamwah alidai kwamba mama huyo wa binti yake alikuwa na mahusiano na jamaa mwingine kwa zaidi ya mwaka mmoja.

"Niligundua alikuwa anatoka kimapenzi na jamaa mwingine kwa zaidi ya mwaka. Kusema kweli wakati wa lockdown nilipokuwa nachoma shati kutokana na msongo wa mawazo alikuwa anaishi kwake. Hiyo ndiyo sababu tulitengana kwa mara ya kwanza," Mulamwah alijibu shabiki aliyehoji kilichosababisha kutengana kwao.

Mulamwah amesema alipogundua mpenzi huyo wake wa zamani alikuwa anamcheza alimwagiza aombe msamaha ila akadai hakuwa tayari kwa hatua hiyo.

"Nilijifanya zuzu, nikaomba msamaha kwa makosa yake, nikamwita na nikaondoka," Alisema.

Mchekeshaji huyo amesema waliporudiana baada ya kutengana kwa mara ya kwanza waliishi kwa upendo mwingi ila hakuwa na amani kutokana na yaliyotokea awali. 

Amedai kwamba alimtema mwigizaji huyo baada ya kuzaliwa kwa binti yao kwani alishindwa kabisa kusahau ya kale.

"Hatukutengana kwa mara ya pili. Tulikuwa tumependana sana. Lakini nilitoka mwenyewe nikaenda baada ya kuzaliwa kwa K. Nilikuwa na mengi kichwani kuhusu yaliyotokea miaka iliyopita na kuona kwamba hangeweza kuomba mssamaha singeweza kusahau. Niliona ni vyema niende," Mulamwah alisema.

Madai ya Mulamwah yanapingana na yale Muthoni aliyosema wakati alipotembelea studio zetu mwezi Februari.

Muthoni alisema alikuwa amempenda sana mchekeshaji huyo na hakuwahi kutoka nje ya mahusiano yao.

"Hatukuwa tunaaminiana. Sikuwahi kuwa na mahusiano ya nje. Sijui kama yeye alikuwa nayo," Muthoni alisema akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni.

Mwigizaji huyo alisema anamheshimu sana Mulamwah na akatoa ombi kwake ampatie  heshima pia.