Propesa apuuzilia mbali madai ya kumpachika mimba aliyekuwa mpenzi wa Mulamwah, Carol Sonnie

Muhtasari

•Propesa amesihi wanablogu kusita kueneza uvumi usio na msingi huku akidai hahusiki kwa namna yoyote katika mzozo wa mtoto huyo wa miezi saba.

Mchekeshaji Propesa na aliyekuwa mpenzi wa Mulamwah, Carol Muthoni
Mchekeshaji Propesa na aliyekuwa mpenzi wa Mulamwah, Carol Muthoni
Image: INSTAGRAM// PROPESA

Mchekeshaji mbali Kimutai Ruto almaarufu Propesa amejitenga mbali na madai kuwa alihusika na ujauzito wa mwigizaji Carol Muthoni.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, Propesa alisema ripoti ambazo zimekuwa  zikienezwa zikidai kuwa yeye ndiye baba mzazi wa bintiye Muthoni ni za uongo.

Propesa amesihi wanablogu kusita kueneza uvumi usio na msingi huku akidai hahusiki kwa namna yoyote katika mzozo wa mtoto huyo wa miezi saba.

"Hii ni hadithi ya uwongo kutoka kwa blogi ghushi. Msiniwekelee mambo sijui hata. Si Mulamwah alisema mahali ilifanyika. Mimi siishi huko. Tafadhali watu wa blogs tafuteni stori ingine," Propesa alisema. 

Mchekeshaji huyo kutoka eneo la bonde la ufa alikuwa anazungumzia ripoti iliyodai kuwa  mzazi mwenza wa Muthoni ni aidha yeye ama Mulamwah.

Wanamitandao wengi walianguka kwenye mtego wa ripoti hizo za uwongo hasa kwa kuwa hapo awali Propesa aliwahi pakia picha yake na Muthoni na kuiambatanisha na ujumbe ulioibua dhana ya mapenzi kati yao.

"Mapenzi ni kitu kilichojaa kujali na hofu-Ovid" Propesa aliandika chini ya picha yake na Muthoni miezi minne iliyopita.

Hata hivyo Muthoni aliwahi kujitokeza na kupuuzilia mbali madai ya mahusiano ya kimapenzi kati yake na mchekeshaji huyo.