Betty Kyallo afichua kilichosababisha kutengana kwake na Nick Ndeda

Muhtasari

•Betty alisema mahusiano yake ya miezi michache na Ndeda yaligonga ukuta baada yao kugundua walikuwa na tofauti nyingi.

•Betty amesisitiza kwamba yeye na Ndeda bado ni marafiki wakubwa licha ya kuwa walitengana mapema mwaka huu.

Nick Ndeda a Betty Kyallo
Nick Ndeda a Betty Kyallo
Image: HISANI

Mtangazaji na mfanyibiashara mashuhuri Betty Kyallo ametupilia mbali uvumi mwingi ulioenezwa kuhusu kilichokatisha mahusiano yake na Nick Ndeda.

Akizungumza katika mahojiano na Dr Ofweneke, Betty alisema mahusiano yake ya miezi michache na Ndeda yaligonga ukuta baada yao kugundua walikuwa na tofauti nyingi.

Mama huyo wa binti mmoja alifichua kwamba yeye na Ndeda walikosa maono sawa kuhusu mahusiano yao.

"Nilipata kumjua, naye alipata kunijua. Tulikuja kugundua kuna mambo kutuhusu ambayo yaligongana. Nadhani ni vizuri kusonga mbele na maisha na kusema ilikuwa halisi," Betty alisema.

Betty aliweka wazi kwamba alifurahia kipindi cha miezi michache ambacho alichumbiana na Nick Ndeda.

"Tulifurahia sana. Tulikuwa marafiki wakubwa. Tulipenda kuwa pamoja sana, tulibarizi pamoja sana, tulienda ziara. Tulikuwa na mahusiano mazuri. Mara zingine mambo hukosa kufanya kazi," Alisema.

Mtangazaji huyo alisema mahusiano yao yalifika kikomo baada ya kuwa pamoja kwa muda na kufahamiana zaidi.

Hata hivyo, Betty amesisitiza kwamba yeye na Ndeda bado ni marafiki wakubwa licha ya kuwa walitengana mapema mwaka huu.

"Namheshimu. Ananiheshimu sana pia. Ni sawa, ni maisha tu," Betty alisema.

Alisema kwamba hayupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mengine na sasa anachukua muda  kuangazia mambo mengine.