Mfanyibiashara Esma Platnumz amefichua kwamba hakuna uhasama wowote kati ya kaka yake Diamond Platnumz na aliyekuwa msanii wake, Harmonize.
Akizungumza na wanahabari katika hoteli ya Hyatt Regency, Esma alidai kuwa vyombo vya habari na mashabiki ndio wamekuwa wakitengeneza ugomvi kati ya wasanii hao wawili ilhali kiuhalisia wao wako sawa.
"Nyinyi ndio mnawagombanisha. Sio wao. Wao wako sawa kabisa," Esma aliwaambia wanahabari.
Mama huyo wa watoto wawili alimtaja Harmonize kama "mtoto" wa Diamond na kusema kakake hawezi kubishana naye.
Aliweka wazi kwamba familia ya Wasafi inafurahia mafanikio ya Harmonize kwa kuwa aliwahi kuwa mmoja wao.
"Tunatamani kumuona Harmonize akipiga hatua kwa sababu ni mtu wetu, ametoka kwetu. Tunafurahi akiwa anazidi kupiga hatua. Hamna kinachotuuma kwa kuwa huyo ni mtu wetu. Diamond hawezi kujibizana na mtoto wake," Esma alisema.
Esma alisema kitendo cha Harmonize kumpatia Diamond tuzo lake kiliashiria kuwa bosi huyo wa Wasafi anaheshimika.