Hatimaye Rayvanny ajiondoa WCB Wasafi na kuzingatia zaidi brand yake ya NLM

Muhtasari

• Hatimaye Rayvanny amevuta utambulisho kwenye bio yake ya Instagram unaomhusisha na lebo ya WCB Wasafi.

Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next level Music, Rayvanny
Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next level Music, Rayvanny
Image: instagram

Staa wa muziki wa bongo fleva na ambaye ni mkurugenzi mkuu mtendaji wa rekodi lebo ya muziki ya Next level Music, Rayvanny ni kama yumo mbioni kuondoka kabisa katika lebo ‘mzazi’ ya WCB Wasafi baada ya muda mrefu wa fununu na uvumi kuenezwa hivyo.

Hili limebainika wazi kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo Rayvanny ameondoa au kufuta baadhi ya maneno yaliyokuwa kwenye bio yake kumtambulisha kama mmoja kati ya wasanii wa lebo ya Wasafi.

Maneno ambayo ameyaondoa kwenye bio yake ni yale yaliyokuwa yakisema “Signed under WCB WASAFI” na sasa bio yake hiyo imebaki kutawaliwa na maneno kama “CEO NLM MUSIC” pekee.

Kwa muda mrefu sasa baada ya msanii Harmonize kuvujisha maongezi baina yake na Rayvanny kuhusu Sakata la kipindi alipokuwa akiondoka Wasafi, msanii Rayvanny amekuwa akionekana kukosa utulivu ndani ya lebo ya Wasafi na mara nyingi kuonesha ishara za kutoka japo uongozi wa lebo hiyo kubwa kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki imekuwa ikikanusha madai hayo.

Harmonize aliporejea nchini Tanzania kutoka ziara yake ya kimuziki nchini Marekani, alivujisha maongezi yake na Rayvanny peupe mbele ya waandishi wa habari kadhaa, maongezi ambayo Rayvanny alisikika akimtetea Harmonize dhidi ya vitendo vya bosi wao Diamond Platnumz na kumsema Simba vibaya kwamba hakuwa anamfanyia Harmonize fadhila kipindi akiwa chini ya Wasafi.