(VIDEO) Gavana Mutua: Sababu za kutozifuta picha za Lilian Ng'ang'a kwenye mitandao yangu ya kijamii

Muhtasari

• Gavana Alfred Mutua amesema hana mpango wowote wa kuzifuta picha za Lilian Ng'ang'a kwenye mitandao yake ya kijamii.

Image: INSTAGRAM//GOVERNOR ALFRED MUTUA

Kama ilivyo kawaida ya wapenzi wengi wanapoachana basi picha zote ambazo walizipakia kwenye mitandao yao ya kijamii wakila maisha kwa vijiko vikubwa zinalishwa kodi nyeusi.

Hali ni tofauti kabisa kwa gavana wa Machakos Dkt. Alfred Mutua ambaye amekiri wazi kwamba hayupo tayari na wala hana mpango wowote wa kuzifuta picha za pamoja walizopiga na aliyekuwa mpenzi wake Lilian Ng’ang’a kutoka katika mitandao yake ya kijamii.

Akizungumza na Nairobi News, Mutua alisema kwamba yeye anaamini Mungu huwakutanisha watu mbalimbali wa makusudi yake mwenyewe na wala hajutii hata sekunde ya miaka 10 ambayo walikipiga pamoja na Ng’ang’a kama wapenzi.

“Hiki ndicho ninachoamini katika maisha, kwamba Mungu huleta watu kwenye maisha yako kwa kipindi chochote ambacho Mungu huchagua na unasherehekea wakati unaotumia na watu hao. Bila kujali matokeo yoyote mabaya au kuanguka, kwa kawaida, ikiwa unatumia muda mrefu na mtu yeyote, kama rafiki, kama mpenzi, kama familia, nyakati nzuri ni bora na zaidi ya nyakati mbaya. Hufurahii tu nyakati nzuri, unasherehekea nyakati nzuri na unakubali nafasi ambayo Mungu amekupa kisha unaendelea na kile ambacho Mungu atakupa na maisha yanaendelea.” alisema gavana Mutua.

Gavana huyo pia alisema kwamba hana mpango pia wa kubadilisha jina la hoteli ya A&L, mgahawa ambao wawili hao walifungua pamoja mjini Machakos enzi za mapenzi yao.

“Jina la hoteli huhifadhiwa isipokuwa Mungu abadilike kwa sababu ni kampuni. Ni mavazi peke yake, sio mtu binafsi. Unajua mimi ni mtu wa moyo mzuri. Mimi sina kisasi au nia mbaya…Nina wema na rehema na ndiyo maana Mungu ananibariki,” Mutua aliweka wazi.

Kinara huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap walitengana na Lilian Ng'ang'a mwezi Oktoba mwaka 2021 ambapo Ng'ang'a alizindua mpenzi wake mpya siku chache baadae. mpenzi huyo mpya akawa ni mwanamuziki wa kufoka Juliani.