Nilikosea sana! Kajala akikubali msamaha wangu, nafunga ndoa naye- Harmonize asema

Muhtasari

•Harmonize alisema uamuzi wa kuomba msamaha  na kumsihi Kajala warudiane ulichanguwa na jinsi mwigizaji huyo alionyesha huruma  licha yake kumkosea.

•Harmonize alitangaza wazi kuwa iwapo mwigizaji huyo atakubali kumsamehe atafunga pingu za maisha naye na kumfanya mkewe.

Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Image: HISANI

Staa wa Bongo Harmonize amesisitiza kuwa anayajuta sana matendo yake yaliyopelekea kuvunjika kwa mahusiano yake na mwigizaji Fridah Kajala Masanja.

Akiwa kwenye mahojiano na E Digital, Harmonize alikiri kwamba hakumkosea Kajala pekee bali familia yake pia.

Mwanamuziki huyo alisema uamuzi wa kuomba msamaha  na kumsihi Kajala warudiane ulichanguwa na jinsi mwigizaji huyo alionyesha huruma  licha yake kumkosea.

"Hebu fikiria iwapo ule muda yeye angeketi chini na waandishi wa habari awaambie ilivyokuwa. Unadhani watu wangenitazama kwa jicho gani? Ingewezekana hata ingeua taaluma yangu ya muziki. Sioni chochote ambacho ninaweza kumlipa. Naamini hata baada ya kuachana yeye ni mmoja wa watu ambao wamekuwa wakiniombea sana na ndio maana nafanikiwa," Harmonize alisema.

Konde Boy aliweka wazi kuwa tayari amefanya mengi katika juhudi za kurejesha uhusiano mwema na mpenzi huyo wake wa zamani. Alisisitiza  hajachoka kuomba msamaha na ataendelea kutia juhudi zaidi akitumai Kajala atakubali ombi lake.

"Suala la yeye kukubali, ni kuhusu yeye na wakati.Imekuwa mwaka mmoja tayari. Huwezi kujua mtu amekuwa akiishi vipi. Mfano mimi nilishasonga mbele na kuwa na Brianna. Siwezi kujua yeye alikuwa katika hali gani. Hata hivyo namshukuru Mungu kwa kuwa anasikia na kuona ninachokifanya," Alisema.

Harmonize alitangaza wazi kuwa iwapo mwigizaji huyo atakubali kumsamehe atafunga pingu za maisha naye na kumfanya mkewe.

"Naamini ananijua zaidi kwa kuwa tumekuwa pamoja. Ikitokea amekubali msamaha wangu na kusema kwamba mimi bado ni mwanaume wake sioni sababu yoyote ya kutomuoa na kumfanya awe mke wangu. Ikitokea hatuko pamoja, angalau nikijua kuwa amenisamehea na moyo wake upo huru itakuwa imetosha kwangu," Alisema.

Wasanii hao wawili walitengana mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa miezi michache tu. Wawili hao walikosana kufuatia madai kuwa Harmonize alijaribu kumtongoza binti wa Kajala wa miaka 19, Paula Kajala.

Baada ya kutengana na Kajala, Harmonize alijitosa kwenye mahusiano na kipusa kutoka Australia, Briana Jai. Hata hivyo wawili hao walitangaza kutengana kwao wiki kadhaa zilizopita.