Kate Actress adokeza kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake

Muhtasari

•Kate alifichua mpango huo wake baada ya kukutana na mwakilishi wanawake wa Muran'ga, Sabina Wanjiru Chege.

•Haya yanajiri huku Sabina Chege akitangaza kwamba hatawania kiti chochote katika uchaguzi wa mwezi Agosti.

Kate Actress na Sabina Chege
Kate Actress na Sabina Chege
Image: INSTAGRAM// KATE ACTRESS

Mwigizaji Catherine Kamau almaarufu Kate Actress amedokeza kuwa ana mpango wa kujitosa kwenye ulingo wa siasa ifikapo 2027.

Kate alifichua mpango huo wake baada ya kukutana na mwakilishi wanawake wa Muran'ga, Sabina Wanjiru Chege.

Mwigizaji huyo ambaye amewahi kupokea tuzo kochokocho kutokana na ubabe wake alidokeza atawania kiti cha mwakilishi wanawake katika kaunti ya Murang'a ama Laikipia.

"Niko na vidokezo vya 2027. Zoea Women Rep wako mapema. Je unajua pia yeye (Sabina Chege)  aliwahi kuwa mwigizaji ? Mtanichagua ama ni mdomo tu? Nisimame wapi, Nyahururu ama Murang'a?" Kate aliandika chini ya picha yake na Sabina ambayo alipakia Instagram.

Kate ni mzaliwa wa eneo la Nyahururu, kaunti ya Laikipia. Mume wake, Philip Karanja naye alizaliwa katika kaunti ya Murang'a.

Haya yanajiri huku Sabina Chege akitangaza kwamba hatawania kiti chochote katika uchaguzi wa mwezi Agosti.

Siku ya Jumamosi Sabina alisema kuwa roho mtakatifu amezungumza naye na kumwagiza aangazie kampeni za Azimio la Umoja tu.

" Hatimaye Roho Mtakatifu amesema, sitagombea nafasi yoyote ya kuchaguliwa katika Kaunti ya Murang'a. Nitazingatia siasa za Kitaifa katika muungano wa Azimio la Umoja. Asanteni wa Murang'a nawapenda sana," Sabina alitangaza.

Sabina ni mmoja wa viongozi wa eneo la Mlima Kenya ambao wanampigia debe kinara wa ODM, Raila Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya.