Ilinichukua miaka 4 kumsamehe Bahati-Yvette Obura

Muhtasari
  • Kwa wakati huo hakukuwa na uhusiano mzuri kati yake na Bahati na hata hawakuwa wanashirikiana katika malezi ya binti yao
Image: INSTAGRAM

Mpenzi wa zamani wa Bahati, Yvette Obura amekiri kuwa alikumbwa na msongo wa mawazo baada yao kutengana na msanii huyo kujitosa kwenye mahusiano na Diana Marua.

Akiwa kwenye mazungumzo na Diana, Yvette alifichua kuwa alikuja kugundua mahusiano mapya ya Bahati na Diana kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa wakati huo hakukuwa na uhusiano mzuri kati yake na Bahati na hata hawakuwa wanashirikiana katika malezi ya binti yao.

"Niliona Baha amesonga mbele na maisha yake nikasema ni sawa. Tulikuwa na ndogo zetu. Tulikuwa wadogo hapo awali na tulikuwa na mipango ya kuwa na familia. Nilijifungua, tukatengana na akapatana na mtu mwingine.  Ikawa nashughulikia mtoto, nauguza jeraha la moyo baada ya kutengana, niko na msongo wa mawazo. Nilishangaa nifanyeje," Yvette alisimulia.

Yvette alisema kwamba baada ya wakati na baada ya kuzungumza naye alielewa kwamba hawezi kumshikilia mtu ambaye hampendi moyoni mwake.

Pia alifichua kwamba ilimchukua miaka 4 kuwasemehe Bahati ni Diana Marua.

"Niliacha kila kitu iende, na ilinichukua miaka 3 kuelekea 4 kusahau kila kitu na kuwasemehe."

Alisema alishangazwa na jinsi mpenzi huyo wake wa zamani aliweza kujitosa kwenye mahusiano mengine haraka.

"Nilijiuliza ni msichana yupi huyo. Nilikufuatilia sana (Diana). Kila siku nilikuwa naamka naanza kuchunguza Diana Marua ni nani. Nilikuwa napitia nikagundua ni msichana ambaye alikuwa kwa video ya wimbo," Alisema.