Mume wangu alikuwa usaidizi na kitia moyo nilichohitaji katika wadi ya leba- Milly Wajesus

Muhtasari

•Milly amesema uwepo wa mumewe  ulimpatia motisha na kumtia moyo alipokuwa anajifungua wiki chache zilizopita.

Image: THE WAJESUS FAMILY YOUTUBE

Mwanablogu Millicent Wambui amemsifu mumewe Peter Kabi kwa kuwa naye katika wadi ya leba alipojifungua mtoto wao wa pili.

Milly amesema uwepo wa mumewe  ulimpatia motisha na kumtia moyo alipokuwa anajifungua wiki chache zilizopita.

"Sijui ningefanya nini bila mume wangu Kabi Wajesus kuwepo katika wadi ya kujifungua. Alikuwa usaidizi na kitia moyo nilichohitaji kwa wakati huo," Milly amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto wawili amesema maombi ya mumewe yalimpatia nguvu alipokuwa anajifungua.

"Shukran kwa kuwa kuhani wa nyumba yetu katika kila hali," Alisema.

Milly na Kabi walitangaza habari za kuzaliwa kwa binti yao mnamo Aprili 8, 2022.

"Utukufu kwa Mungu binti yupo hapa nasi. Ni mzuri, buheri wa afya na ameleta raha kubwa katika maisha yetu. Shukran Kabi Wajesus kwa kuwa mwenza bora wa kukuza familia naye," Milly alitangaza kupitia Instagram.

Wanandoa hao walirekodi safari ya ujauzito wao hadi  kujifungua na wamekuwa wakipakia video hizo kwenye Youtube.

Mojawapo wa tukio ambalo walirekodi ni lile la kujifungua. Video walizopakia Youtube zimeonyesha kuwa Kabi alishuhudia mkewe akisaidiwa na wauguzi kujifungua.

Wanamitandao wametoa hisia tofauti kuhusiana na suala la Kabi kuwepo kando ya mkewe wakati alikuwa anajifungua. 

Baadhi wamemsuta mwanavlogu na mfanyibiashara huyo huku wengine wakiunga mkono jambo hilo.