Bahati alimfanyia binti yetu kipimo cha DNA- Yvette Obura afichua

Muhtasari

•Yvette alisema Bahati alikuwepo wakati alikuwa anajifungua binti huyo wao ila wakakosana baadae na kutengana.

•Diana Marua kwa upande wake alisema alijaribu kumzuia mumewe Bahati dhidi ya kufanya vipimo vya DNA.

Yvette Obura, Bahati na binti yao
Yvette Obura, Bahati na binti yao
Image: INSTAGRAM// YVETTE OBURA

Mpenzi wa zamani wa Bahati, Yvette Obura amefichua kwamba mwanamuziki huyo aliagiza kufanyika kwa vipimo vya DNA kubainisha iwapo ni kweli yeye ndiye baba ya binti yake.

Yvette alifichua hayo akiwa kwenye mahojiano na mke wa sasa wa Bahati wakati ambapo walikuwa wanazungumzia suala la kushirikiana kwao katika malezi.

Malkia huyo ambaye walitengana na Bahati zaidi ya miaka mitano iliyopita amedai mwanamuziki huyo alifanya vipimo hivyo ila hakuwahi kumwambia matokeo.

"Alifanya DNA lakini sijawahi kujua matokeo ama kitu chochote. Siku moja alinipigia akaniambia anataka Mueni ili waende wakapigwe picha. Hiyo ni ishara kuwa matokeo ya DNA yalithibitisha yeye ndiye baba," Yvette alisema.

Diana Marua kwa upande wake alisema alijaribu kumzuia mumewe Bahati dhidi ya kufanya vipimo vya DNA.

"Bahati alitaka kufanya DNA na mtoto. Kwa kweli hilo lilileta shida. Mimi sikuwa nimewahi kuona mtoto huyo lakini nilijua yupo. Nilisema uamuzi ni wake, kama hilo ndilo lingefanya atulie nilisema ni sawa," Diana alisema.

Diana amesema alipomwona mtoto huyo kwa mara alimbainishia mumewe kuwa ni wazi yeye ni damu yake.

"Nilimwambia huyu mtoto ni wewe kabisa, ako na sifa zako nyingi," Alisema.

Diana aliweka wazi kuwa Bahati alipoanza kumchumbia alimfahamisha kuwa ana binti ambaye alikuwa amepata na mpenzi wake wa zamani.

Yvette alisema Bahati alikuwepo wakati alikuwa anajifungua binti huyo wao ila wakakosana baadae na kutengana.

Hata hivyo wameendelea kushirikiana vizuri katika malezi. Kwa sasa Yvette na Diana ni marafiki wazuri licha ya tofauti zao za hapo awali.