Ni mzee anayejijenga na watoto!" Njugush amkosoa vikali Andrew Kibe

Muhtasari

•Njugush alimkosoa mtangazaji huyo kwa kuingilia maisha na kazi za wasanii chipukizi wanaotia bidii katika kazi zao.

•Mchekeshaji huyo alisema Kibe anapendelea kumulika makosa ya wengine na kuyafumbia macho makosa yake.

Andrew Kibe , Blessed Njugush
Andrew Kibe , Blessed Njugush
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Timothy Kimani almaarufu Njugush amemkashifu vikali Andrew Kibe kwa kuwakosoa wasanii wengine.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Njugush alimshutumu mtangazaji huyo kwa kujaribu kuwashusha wasanii chipukizi.

Mchekeshaji huyo alisema Kibe anapendelea kumulika makosa ya wengine na kuyafumbia macho makosa yake.

"Nikimuangalia naona mtu ambaye amepotea. Hakuna kinachofanya kazi kwake. Anasema anataka kuweka watu laini, yeye kwanza yupo laini?.. Nitasema bila shaka, naweza kuwa nimefanya makosa mengi maishani lakini sitawahi kufanya makosa kama ambayo amefanya. Nilipo najua nimefanikiwa na mengi kuliko ambayo Kibe atawahi kupata," Njugush alisema.

Njugush alimkosoa mtangazaji huyo kwa kuingilia maisha na kazi za wasanii chipukizi wanaotia bidii katika kazi zao.

"Yeye ni mzee ambaye anajijenga na watoto. Kwa nini tufurahie kuwashusha wengine na kuona mabaya tu? Hata kitabu chasema utupe mawe ikiwa tu wewe ni msafi. Sisi wote tuko na shida zetu. Hata hivyo nafurahia kuwa tunafanya makosa yetu tukiwa na umri mdogo," Alisema.

Mchekeshaji huyo alisema sio vizuri kupigana na vijana kwa sababu ya makosa yao huku akidai kuwa bado wana muda mwingi wa kuyarekebisha.

Aliwashauri vijana kutoogopa kupiga hatua wanazoamini zitawaletea mafanikio maishani kwa hofu ya kusemwa na jamii.

Kibe anajulikana kuwakosoa watu mbalimbali hasa wasanii kupitia YouTube channel yake na mitandao ya kijamii.