Tunajaribu kumtafutia Butita mke- Njugush na mkewe wafichua

Muhtasari

•Njugush alisema wamekuwa wakijaribu kumuunganisha Butita na vipusa kadhaa wakitumai ataweza kutongoza mmoja wao na kujitosa kwenye mahusiano naye.

•Bi Ndinda alisema marafiki wengi wa karibu wa mumewe ni wanafamilia isipokuwa Butita ambaye wanajaribu kutafutia mke.

Image: INSTAGRAM// CELESTINE NDINDA

Mchekeshaji Blessed Njugush na mke wake Celestine Ndinda wamefichua kuwa wapo katika harakati za kumsaidia msanii mwenzao Eddie Butita kupata jiko.

Wawili hao walifichua hayo wakiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz ambapo walizungumzia masuala mbalimbali kuhusu maisha yao.

Njugush alisema wamekuwa wakijaribu kumuunganisha Butita na vipusa kadhaa wakitumai ataweza kutongoza mmoja wao na kujitosa kwenye mahusiano naye.

"Tunajaribu hata kumchokozesha watu. Unapita hapo tunakuita. Tunajaribu lakini atashika rada. Mungu atamuonekania. Juzi tumejaribu tumuunganisha na kasichana kazuri nikamwambia huyu anaitwa Butita na hana mtu, Butita akasema ni kweli hana mtu kwa sasa, sijui wamefikishana wapi lakini tunatumai atafika hapo," Njugush alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa kwa kawaida Butita huwa anawaza na kufanya kana kwamba yupo kwenye ndoa.

Bi Ndinda alisema marafiki wengi wa karibu wa mumewe ni wanafamilia isipokuwa Butita ambaye wanajaribu kutafutia mke.

"Butita tunajaribu kumtafutia mtu. Atapata," Ndinda alisema.

Sio mengi yanayojulikana kuhusu mahusiano ya mchekeshaji Eddie Butita.

Kwa muda mrefu hata hivyo kumekuwa na tetesi kuwa msanii huyo yupo kwenye mahusiano na mchekeshaji mwenzake Mamito.

Wiki kadhaa zilizopita kulikuwa na uvumi kuwa kwa sasa Mamito amebeba ujauzito wa mchekeshaji huyo wa Churchill Show.  Butita alipohojiwa hakukiri wala kukana madai hayo.