Mama yangu anampenda aliyekuwa mume wangu Jared- Akothee afichua

Muhtasari

•Akothee alieleza kuwa mama yake ana upendo mwingi sana kwa mume wake wa zamani Jared Otieno.

•Jumapili Akothee aliandamana na mamake, nyanya yake na wanafamilia wengine kuenda kufariji familia ya kina baba wa binti zake watatu

Akothee na Jared Okello
Akothee na Jared Okello
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku chache zilizopita mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee alijumuika na familia ya aliyekuwa mumewe Jared Otieno kumzika baba yake Evans Otieno.

Akothee aliandamana na familia yake wakiwemo mama yake na binti zake wawili Vesha Okello na Rue Baby.

Alieleza kwamba licha ya kuwa ndoa yake na Jared haikufua dafu bado anasalia kuwa mmoja wa familia yao na ndio maana akaungana nao.

"Mwanamke yeyote ambaye aliwahi kuolewa katika familia fulani na ana watoto kutoka kwa familia hiyo, kuna sababu kwa nini uko katika familia hiyo. Leteni umoja na sio mgawanyiko, upendo na sio chuki. Ikumbatie familia mpya ambayo Mungu amekupa. Familia imeundwa na Mungu, uhusiano unajengwa na Mungu, na urafiki unafanywa na wanadamu. Kutana na familia yangu iliyofiwa. Mama yangu na familia yangu pia walikuja kutufariji," Akothee alisema kupitia Instagram.

Akothee aliendelea kueleza kuwa mama yake ana upendo mkubwa sana kwa mume huyo wake wa zamani. Alidokeza kuwa mama yake angefurahia zaidi kumuona bado katika familia ya kina Jared.

"Weeee niseme nini tena baada ya Mungu kupatia mama wa ajabu kwa mwanamke mzuri kama mimi‼️ Ash mapenzi mama yangu anayo kwa Ex wangu, naapa kama angekuwa na uwezo wa kuniweka hapa kwa nguvu, angeyasikiliza maneno yake yenye nguvu," Akothee aliandika chini ya video ya mamake akizungumza katika mazishi ya babake Jared.

Akitoa hotuba yake, mamake Akothee alifichua kuwa yeye ndiye aliyemshinikiza bintiye kununua kipande cha shamba na kujenga karibu na wakwe wake.

"Nilipokuja kutembelea mzee (babake Jared), alinisihi niambie binti yangu aje ajenge nyumba. Nilimwambia Esther aje anunue kipande cha shamba hapa.. Hakuna kitu unachoweza kusema kati ya binti yake na wakwe wako," Mamake Akothee alisema.

Jumapili Akothee aliandamana na mamake, nyanya yake na wanafamilia wengine kuenda kufariji familia ya kina baba wa binti zake watatu