"Nakupenda mziwanda wangu" Khadija Kopa ajivunia baada ya bintiye Zuchu kumsherehekea

Muhtasari

•Kopa amemshukuru bintiye kwa jinsi alivyomsherehekea na kuonyesha upendo wake kwake katika siku hiyo maalum kwa kina mama.

•Zuchu alimtakia mamake kheri za siku ya kina mama na kumhakikishia kuhusu upendo wake mwingi kwake.

Khadija Kopa na Zuchu
Khadija Kopa na Zuchu
Image: INSTAGRAM

Malkia wa mipasho Khadija Kopa ameshindwa kuzuia furaha yake baada ya binti yake Zuchu kumsherehekea kwa zawadi kemkem mnamo Mother's Day.

Bi Kopa amemshukuru bintiye kwa jinsi alivyomsherehekea na kuonyesha upendo wake kwake katika siku hiyo maalum kwa kina mama.

"Ahsante sana mwanangu kwa kuthamini uwepo wangu. Nakupenda mziwanda wangu Zuchu," Bi Kopa alimwandikia bintiye kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo mkongwe aliambatanisha ujumbe wake na video ya zawadi alizopokea kutoka kwa Zuchu.

Zawadi ambazo Zuchu alimtumia mamake ni pamoja na nguo, mashuka, maua na ujumbe mtamu wa Mother's Day. 

Katika barua yake, Zuchu alimtakia mamake kheri za siku ya kina mama na kumhakikishia kuhusu upendo wake mwingi kwake.

"Happy Mother's Day. Nakupenda na asante kwa yote Mama yangu. Hakuna mwingine kama wewe," Barua ya Zuchu ilisoma.

Zuchu ni kitinda mimba wa Khadija Kopa ambaye aliwahi kubarikiwa na watoto wanne kwa jumla.

Familia ya Kopa ni familia ya muziki kwani yeye na watoto wake wote ni wasanii ikiwemo marehemu Omari Kopa ambaye aliaga dunia 2007.