Nina sifa nzito, Mahari yangu ni milioni 2- Aliyekuwa mpenzi wa Simple Boy, Pritty Vishy atangaza

Muhtasari

•Vishy aliweka wazi kuwa hataki mume wake mtarajiwa awape wazazi wake ng'ombe kama mahari yake.

•Amesema mwanaume anayemtamani ni sharti awe tajiri, awe tayari kumpa heshima anayostahili na awe Mcha Mungu.

Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Mpenzi wa zamani wa mwanamuziki Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy ametangaza kuwa mwanaume anayekusudia kumuoa ni sharti awe tayari kulipa mahari ya shilingi milioni mbili.

Akiwa kwenye mahojiano na Nicholas Kioko, Vishy aliweka wazi kuwa hataki mume wake mtarajiwa awape wazazi wake ng'ombe kama mahari yake.

Kipusa huyo amesema mume wake mtarajiwa anapaswa kuwapatia wazazi wake gari badala ya ng'ombe.

"Mahari yangu ni milioni mbili. Na mtu asijaribu kuniletea ng'ombe. Sitaki ng'ombe zinaletwa kwetu. Mimi ni milioni mbili, tosha! Kama unataka kuleta ng'ombe basi hiyo pesa ununue gari. Hiyo pesa ya ng'ombe unafaa kuchanga ununue gari ulete," Vishy alitangaza.

Vishy amesema kuwa ana sifa kemkem zinazofanya astahiki kiasi hicho kikubwa cha fedha kama mahari.

"Sifa zangu ni nzito, ata mimi ni mzito. Mi ni mzito, najua kupika, najua kukanda. Nina sifa nyingi," Alisema Vishy.

"Siwezi kulima. Sitaki kuzirai kwa shamba. Ulioa nilime ama ulinioa niwe bibi yako," Aliongeza.

Vishy ameweka wazi kuwa bado hajapata mchumba ambaye anakusudia kujitosa kwenye ndoa rasmi naye.

Amesema mwanaume anayemtamani ni sharti awe tajiri, awe tayari kumpa heshima anayostahili na awe Mcha Mungu.

"Ningetaka mwanaume mwenye ako na pesa. Mimi hutanioa nikuje niteseke. Lazima ukuwe na pesa. Pili ni sharti uwe unaniheshimu. Pia awe anamheshimu Mungu. Hizo zingine tutatafuta," Alisema.

Vishy alikuja kutambulika zaidi mapema mwaka huu kutokana na mahusiano yake na Stivo Simple Boy. Mahusiano yao yalifichuka hadharani baada ya video yao ambayo kipusa huyo alipakia kwenye TikTok kuvuma.

Baadae Vishy alifichua kuwa walijuana na mwanamuziki huyo zaidi ya miaka mitano iliyopita na urafiki wao ukakua kuwa mahusiano.  Wawili hao hata hivyo walitangaza kutengana kwao mwezi uliopita.