Mchekeshaji Vincent Mwasia almaarufu Chipukeezy amefunguka kuhusu madai ya mzozo kati yake na aliyekuwa mshirika wake Kartelo.
Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Chipukeezy alisema hajawahi kuwa na shida yoyote na mchekeshaji huyo mwenzake.
Msanii huyo kutoka Machakos alimtambua Kartelo kama rafiki yake mkubwa ambaye wamepitia mengi pamoja naye.
"Kartelo ni kijana mmoja ambaye najivunia. Ni mtu ambaye nyota yake inang'aa. Ni mtu mbunifu, mwenye talanta na mjanja sana. Kartelo na mimi hatujawahi kuwa na shida nikiongea kutoka moyoni mwangu. Ata yeye anajua kuwa kama kuna mtu ameweka maslahi yake moyoni ni mimi, tumepitia mengi pamoja. Kartelo ni rafiki yangu," Chipukeezy alisema.
Mchekeshaji huyo hata hivyo alikiri kuwa kuliwahi kutokea tofauti kati yake na Kartelo ingawa alisita kuzizungumzia.
Alifichua kuwa yeye na Kartelo wamewahi kushirikiana katika mambo tofauti, sio ya kikazi tu bali pia ya kimaisha.
Chipukeezy alisema familia yake inampenda sana mfanyikazi mwenza huyo wake wa zamani kwa kuwa amewahi kusimama nao katika nyakati ngumu.
"Babu yangu alipoaga, Kartelo ndiye msanii pekee ambaye alihudhuria mazishi yake. Alikuja akakaa nasi, kila mtu katika familia yangu wanampenda Kartelo. Wanamuona kama ndugu. Kulingana nai, hatuwezi kukosana na Kartelo, Kartelo ni rafiki yangu. Ni mtu ambaye licha ya tofauti tunazoweza kuwa nazo tutabaki kuwa familia. Sisi ni familia kubwa," Alisema.
Chipukeezy hata hivyo alikiri kuwa hajaweza kuwasiliana na baba huyo wa mtoto mmoja kwa muda mrefu. Alisema kuwa hajajaribu kumfikia kwa kuwa bado anampatia muda wa kushughulikia masuala yake binafsi.
Aidha mchekeshaji huyo alitangaza kuwa anamtafuta Kartelo ili waweze wafanye kazi pamoja tena.
"Chukua muda wako. Kuwa wewe. Bora uko na talanta, ukijitokeza utavuma. Chukua muda wako. Fanya usanii wako kiwewe. Na unipigie simu," Alisema.