Mulamwah azungumzia suala la kurudiana na Carrol Sonnie

Muhtasari

•Mulamwah alisema kwa sasa kila mmoja wao anaangazia kazi zake baada yao kupoteza sana walipokuwa wanarumbana.

•Takriban mwezi mmoja uliopita, wazazi wenza hao wawili walionekana pamoja katika video ambayo walipakia Instagram.

Image: INSTAGRAM/CAROL SONNIE

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amesema hawezi kubashiri ikiwa yeye na aliyekuwa mpenzi wake Carol Muthoni watawahi kurudiana.

Akiwa kwenye mahojiano na Presenter Ali, Mulamwah hata hivyo aliweka wazi kuwa yeye na Muthoni waliamua kutoendelea kugombana hadharani.

Baba huyo wa mtoto mmoja alisema kwa sasa kila mmoja wao anaangazia kazi zake baada yao kupoteza sana walipokuwa wanarumbana.

"Saa hizi watu wanaangazia mambo mengine. Tuliona yale tulliyokuwa tunafanya yalikuwa yanaturudisha nyuma sana na watu walikuwa wanaichukulia kama burudani. Tulikuwa tunang'ang'ana kuonyesha ni nani mzuri. Mwisho wa siku hatukuwa tunatengeneza pesa sisi na tulikuwa tunajiharibia jina," Alisema Mulamwah.

Mchekeshaji huyo alikiri kuwa yeye, Muthoni na binti yao walipoteza dili na fedha nyingi katika kipindi ambacho walikuwa wanajibizana hadharani.

Aidha alifichua kuwa video ambayo walifanya pamoja mwezi uliopita ililenga kuleta utulivu kati yao.

"Cha muhimu zaidi ni kutulia na kurudi kazi. Hiyo ndiyo ilikuwa lengo ya video ambayo tulifanya," Alisema.

Takriban mwezi mmoja uliopita, wazazi wenza hao wawili walionekana pamoja katika video ambayo walipakia Instagram.

Video hiyo ilichochea mdahalo mkubwa miongoni mwa wanamitandao huku baadhi wakiwashtumu wawili hao kwa kutafuta kiki.

Mulamwah hata hivyo ametupilia mbali madai ya kiki huku akidai kuwa huwa ametathmini hali ilivyo kabla ya kutekeleza jambo fulani.

"Mimi huwa sitafuti kiki. Kabla nichapishe lolote huwa nimetathmini hali zote. Huwa natathmini matokeo yoyote. Kila kitu huwa imepangwa vizuri. Vitu mnaona saa hii zilipangwa takriban mwaka mmoja uliopita," Alisema.

Mchekeshaji huyo pia alikana kuwa alikuwa anatafuta kiki wakati alipodai kuwa yeye sio baba mzazi wa binti ya Sonnie.