Harmonize apuuzilia mbali madai kuwa magari aliyomnunulia Kajala yamesajiliwa kwa jina lake

Muhtasari

•Harmonize amelazimika kuonyesha kadi za magari hayo kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa wakosoaji wake.

•Juma Lokole alikuwa ameibua madai kuwa Harmonize alikuwa anatafuta kiki tu kwa suala lote la kumnunulia Kajala gari.

Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amejitokeza kupuuzilia mbali madai kuwa magari mawili anayodai kuwa alimnunulia Kajala yamesajiliwa kwa jina lake.

Harmonize amelazimika kuonyesha kadi za magari hayo kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa wakosoaji wake.

Kupitia ukurasa wake alionyesha kadi kutoka kwa Mamlaka ya Ushuru nchini Tanzania ambayo imeandikishwa kwa jina Frida Kajala Masanja.

Harmonize aliambatisha picha ya kadi hiyo na ujumbe ambao ulionekana kumkejeli mtangazaji Juma Lokole ambaye alikuwa ameibua madai kuwa Kajala alikataa kupokea gari hilo baada ya mpenzi huyo wake wa zamani kukosa kuonyesha jina lililoandikishwa kwenye kadi.

"Ndugu yangu hakikisha kuwa umempatia kadi kabla ya kifunguo. Kama umapenda kweli na upo tayari kufa kuzikana kwa nini umpe gari umwambi la kwake alafu kadi inasoma jina lako na la ukoo wako. Acha kucheza unajihadaa . Na nini hutaki kuandika jina lake kwenye kadi au ya ndugu zako umeiegesha tuu kwa mtoto wa watu. Akifa anyang'anywe. Hata hivyo nakupenda mwanamke bosi wa maisha yangu. Hii ni yako," Harmonize aliandika juu ya picha ya kadi  hiyo.

Hapo awaliJuma Lokole alikuwa ameibua madai kuwa Harmonize alikuwa anatafuta kiki tu kwa suala lote la kumnunulia Kajala gari.

Juma alisema baada ya magari mawili aina ya Range Rover aliyonunua Harmonize kutua nchini Tanzania yalipelekwa nyumbani kwa Kajala ila yakakataliwa.

"Ile gari ilipelekwa hadi kwa Kajala. Kajala ana akili. Ilifikishwa hadi pale kisha lango likafungwa wakaambiwa warudishe uchafu walikotoa. Mwanadada mmoja alitoka nje na kusema hawahitaji gari, ila wanahitaji kadi ya gari ili kuona imeandikwa jina gani? Alisema mwambieni alete kadi ya hilo gari yenye imeandikwa Kajala. Sio gari, alete kadi imeandikwa  Kajala. Ukileta kadi tutapokea tukubali msamaha," Juma alisema akiwa kwenye mahojiano na Bingo Online Tz.

Mtangazaji huyo wa Wasafi Media alidai kuwa magari ambayo Harmonize alinunua hayakuwa mapya kwani tayari yalikuwa yametumika.

Alisema kuwa Kajala ana ufahamu mkubwa kuhusu magari na alijua kuwa bosi huyo wa Kondegang Music Worldwide alikuwa anamchenga.