Mama ya Hamisa Mobetto afichua mambo ambayo bintiye huzingatia kwa mwanaume

Muhtasari

•Bi Lutigunga alisema ni wanaume wengi ambao wamewahi kuenda kwake  wakijaribu bahati yao kwa binti yake.

•Litigunga ameeleza kuwa wanaume wengi wamekuwa wakifeli kuteka moyo wa bintiye  kwa kuwa hawapo tayari kukubali watoto wake.

Hamisa Mobetto na Mamake
Hamisa Mobetto na Mamake
Image: HISANI

Bi Shufaa Lutigunga amefichua kuwa kufikia sasa amepokea posa nyingi kutoka kwa wanaume wanaommezea mate binti yake Hamisa Mobetto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa EP ya bintiye, Bi Lutigunga alisema ni wanaume wengi ambao wamewahi kuenda kwake  wakijaribu bahati yao kwa binti yake.

"Kazi yangu ni kupokea posa. Posa nimekula nyingi. Ata leo nimekula posa. Wakati yeye anahojiwa huko mimi nimekula posa," Lutigunga aliambia waandishi wa habari.

Licha ya kuwa wanaume wengi wamewahi kujitokeza kuomba ndoa na Hamisa, mama yake amefichua kuwa amekuwa makini sana katika suala la mahusiano yake.

Amesema chaguo la bintiye la mpenzi ni mwanaume ambaye atampenda jinsi alivyo bila kubagua chochote ikiwemo watoto wake wawili.

"Hamisa ni mtu mwenye tabia tofauti. Kuna wanaume ambao wanakuja wakimtaka. Lakini Hamisa ana watu ambao wanamzunguka. Ana watoto  wawili ambao wana baba wawili tofauti. Je, uko tayari kumpenda yeye pamoja na watoto wake wawili," Alisema

Litigunga ameeleza kuwa wanaume wengi wamekuwa wakifeli kuteka moyo wa bintiye  kwa kuwa hawapo tayari kukubali watoto wake.

"Unakuta wanaume wengi labda anampenda Hamisa hapendi watoto wake. Wengine labda wanatofautiana na baba mmoja. Vitu kama hivo. Huwa anaangalia vitu vingi. Anataka mwanaume ampende jinsi alivyo," Alisema.

Aidha Mama Mobetto alisema bintiye amekuwa makini kwa kuwa anahofia sana kujipata kwenye ndoa ambapo ataishia kunyanyasika.

Pia aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kumsukuma binti yake kuwa kwenye ndoa ambayo mwenyewe hajataka.

"Mimi ni mama tofauti kabisa. Siwezi kumsukuma mwanangu. Anataka apate pesa kwanza ndiposa akiolewa asinyanyasike. Wanawake wengi wananyasasika kwenye ndoa. Wengi wanaolewa na wanaume tajiri wakiwa na umri mdogo kisha wanadhalilika kila siku. Hamisa hataki hicho kitu kitokee," Alisema.

Hamisa amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata kupata watoto na wanaume wawili maarufu.

Mtoto wa kwanza wa mwigizaji na mwanamuziki huyo, Fantasy Majizzo alizaliwa mwaka wa 2015. Fantasy ni binti ya Hamisa na mfanyibiashara  Francis Ciza Majizzo.

Mobetto pia ana mtoto wa kiume na bosi wa WCB Diamond Platnumz ambaye alikuwa kwenye mahusiano naye miaka ya hapo awali. Mtoto wa Hamisa na Diamond anajulikana kama Dylan.