"Mwili ni mfupa tupu" Eric Omondi afunguka jinsi Rais Kenyatta alivyomchochea kujenga mwili

Muhtasari

•Eric amesema rais alielezea wasiwasi wake kuhusu saizi ya mwili wake wakati walipokutana naye takriban miaka minne iliyopita.

• Mabadiliko makubwa katika saizi ya mwili wa Eric Omondi yameweza kuonekana  tangu mwaka huo wa 2018

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji maarufu Eric Omondi amefichua kuwa alianza harakati za kujenga mwili wake baada ya kuchochewa na rais Uhuru Kenyatta.

Eric amesema rais alielezea wasiwasi wake kuhusu saizi ya mwili wake wakati walipokutana naye takriban miaka minne iliyopita.

Amesema siku hiyo itasalia kuwa kumbukumbu kwa kuwa hiyo ndio siku ambayo alifanya maamuzi ya kubadilisha mpango wake wa chakula na kununua vifaa vya mazoezi.

'Sitasahau siku hii. likuwa tarehe 13 Mei 2018. Rais alinishika mabega, akanitazama moja kwa moja machoni, akanitikisa mara tatu na kusema "Kula Bwana, Mwili ni mfupa tupu". Siku hiyo nilienda nyumbani nikafanya mpango wa chakula na kununua chumba cha mazoezi. Mengine ni Historia," Omondi alisema kupitia Instagram.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha ujumbe huo  na picha yake na rais Kenyatta akiwa amemshika mabega.

Ama kweli mengine ni historia kwa kuwa mabadiliko makubwa katika saizi ya mwili wa Eric Omondi yameweza kuonekana  tangu mwaka huo wa 2018.

Mara  nyingi Omondi ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuonyesha misuli yake na kifua kilichotokea.

Kutumbuiza bila shati umekuwa mtindo wake katika miaka ya hivi majuzi pengine akilenga kujigamba kuhusu mwili wake.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 40 pia anajulikana kuwa mgeni wa mara kwa mara wa chumba cha mazoezi.

Kutokana na kukua kwa mwili wake Eric amekuwa akiitisha pambano la nguvu hadharani dhidi ya wasanii wenzake waliojenga ila mara nyingi ameishia kushindwa.

Hivi majuzi alibwagwa chini na staa wa Bongo Harmonize katika kinyang'anyiro walichoonyesha kupitia Instagram. Hii ina maana kuwa mchekeshaji huyo bado ana kibarua kikubwa zaidi cha kufanya.