Hamisa Mobetto azungumzia suala la kutoka kimapenzi na Rick Ross

Muhtasari

•Hamisa Mobetto ameweka wazi kuwa uhusiano wake na Rick Ross ni wa kirafiki tu na haijawahi kutokea zaidi ya hicho.

•Amefichua kuwa Rick Ross amekuwa nguzo muhimu katika taaluma yake ya usanii kwa kuwa amekuwa akimsaidia kwa ushauri.

Hamisa Mobetto na Rick Ross
Hamisa Mobetto na Rick Ross
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki na muigizaji wa Bongo Hamisa Mobetto amefafanua zaidi uhusiano wake na rapa wa Marekani Rick Ross.

Akiwa kwenye mahojiano katika Clouds Media, Mobetto alisisitiza kuwa hajawahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na rapa huyo tajika.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz aliweka wazi kuwa uhusiano wake na Rick Ross ni wa kirafiki tu na haijawahi kutokea zaidi ya hicho.

"Hakujawahi kuwa na mahusiano. Huwa ananipa makopakopa kwa sababu nafanya naye kazi. Hakuna chochote. Pindi kikitokea kama kuna kitu mtafahamu," Mobetto alisema. 

Mobetto hata hivyo alifichua kuwa Rick Ross amekuwa nguzo muhimu katika taaluma yake ya usanii kwa kuwa amekuwa akimsaidia kwa ushauri. Alisema kuwa anavutiwa sana na muziki wa Ross.

Alifichua kwamba licha ya kuwa hajamshirikisha rapa huyo kwenye wimbo wowote katika EP yake, kuwa tayari kuna kitu wamewahi kufanya pamoja ambacho ataachia siku za baadae.

"Yeye ni mtu ambaye ananisapoti. Ana moyo wa kusaidia," Mobetto alisema.

Mama huyo wa watoto wawili ameonekana kuwa na uhusiano wa karibu sana na Rick Ross hasa katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho kimepita. Wengi wamekuwa wakishuku kuwa huenda uhusiano wao ni zaidi ya urafiki hasa kutokana na upendo mkubwa ambao wamekuwa wakionyeshana kwenye Instagram.

Katika mahojiano hayo Mobetto pia alifichua kuwa ni wanaume wengi ambao wamewahi kufika kwao na kutoa posa katika juhudi za kufunga ndoa naye. Alifichua kuwa posa ya chini zaidi ambayo imewahi kufika kwao ilikuwa ya Tsh10m.

"Ndogo zaidi ilikuwa ya 5M. Lakini ya 5M haikutufikia. Ambayo ilifika nyumbani ya chini zaidi ilikuwa Milioni 10," Alisema.

Mobetto amekuwa akiahirisha posa hizo kutokana na masuala mbalimbali yakiwemo kukosa kufahamiana vizuri na wanaume hao. Hata hivyo alifichua kuwa kuna mwanaume mmoja kati yao ambao aliteka moyo wake nusura wafunge ndoa naye.