Muigizaji Serah Teshna afunguka kuhusu kuishi pamoja na mchumba wake Victor Wanyama

Muhtasari

•Serah Teshna amefichua kuwa  amekuwa akiishi pamoja na nahodha huyo wa zamani wa Harambee Stars.

•Muigizaji huyo amefichua kuwa amekuwa akipumzika kuigiza tangu alipojifungua na tayari  amejenga uhusiano mkubwa na mwanawe.

Serah Teshna na mchumba wake Victor Wanyama
Serah Teshna na mchumba wake Victor Wanyama
Image: HISANI

Muigizaji maarufu Serah Teshna ameweka wazi kwamba hayupo kwenye mahusiano ya umbali mrefu na mchumba wake Victor Wanyama.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Serah alifichua kuwa  amekuwa akiishi pamoja na nahodha huyo wa zamani wa Harambee Stars.

Mbabe huyo wa uigizaji ambaye yupo nchini kwa sasa alisema amerejea hapa Kenya kwa minajili ya kikazi tu.

"Sipo kwenye mahusiano ya umbali mrefu. Kusema kweli tumekuwa pamoja kila wakati, tunaishi pamoja. Niko hapa kwa sababu ya kazi ninayofanya hapa kisha nirudi," Serah alisema.

Kwa sasa Wanyama anaishi Canada ambapo anachezea klabu ya CF Montreal inayoshiriki katika Major League Soccer (MLS).

Serah amesema kuwa anakusudia kuungana tena na familia yake punde baada ya kukamilisha kazi iliyomleta hapa nchini.

"Huwa hatuweki mambo yetu wazi lakini daima tuko pamoja katika kila jambo. Niko hapa kwa mradi huu tu lakini baada ya kumaliza ni lazima niungane tena na familia yangu," Serah alisema.

Muigizaji huyo alisema anatazamia sana kuungana tena na nyota huyo wa kandanda.

Serah na Wanyama walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja Septemba mwaka jana. Serah alitangaza habari za kuzaliwa kwa mtoto wao wa kiume siku 40 baada ya kujifungua.

“2021. Mungu alijitokeza na Kujionyesha. Tunayo furaha kushiriki safari hii ya ajabu na wewe. Mungu ndiye mkuu. #siku40ZaBabyCuddles," Teshna alitangaza mwezi Oktoba kupitia Instagram.

Muigizaji huyo amefichua kuwa amekuwa akipumzika kuigiza tangu alipojifungua. Amesema kuwa ana uhusiano wa karibu sana na mwanawe.