(+Video) Mwigizaji Omosh atolewa mapepo na Pastor Kanyari hadi kuanguka chini

Muhtasari

•Omosh alisema yupo tayari kutengeneza madhabahu yake na Mungu vizuri baada ya kusikiliza mahuburi ya Kanyari.

•Kanyari aliwekelea mkono wake kwenye utosi wa Omosh na kuanzisha maombi ambayo yaliishia kwa mwigizaji kuanguka chini kwa mgongo.

Mwigizaji Joseph Kinuthia almaarufu Omosh amekuwa gumzo tena mitandaoni baada ya video yake akianguka wakati akiombewa na mhubiri mashuhuri Victor Kanyari kusambaa.

Katika video hiyo Omosh anaanza kwa kujitambulisha kisha anaendelea kueleza jinsi alivyojipata katika kanisa la Kanyari.

Mwigizaji huyo wa Tahidi High alieleza kuwa aliamua kupiga hatua hiyo baada ya rafiki yake kumshawishi ahudhurie ibada ya kanisa. Baada ya ibada ndipo Kanyari alimpatia msanii huyo nafasi ya kutoa ushuhuda wake.

"Leo nimesoma kuhusu madhabahu. Nikiwa nimekaa pale chini nimeona labda mambo yangu huenda mrama kwa kuwa sijajenga madhabahu vizuri. Hapa nimesoma lazima nijenge madhabahu yangu ili naye Mungu ashuke anene nami," Omosh alisema mbele ya waumini waliokuwa wamejumuika pale kanisani.

Omosh alisema yupo tayari kutengeneza madhabahu yake na Mungu vizuri baada ya kusikiliza mahuburi ya Kanyari.

Kanyari alipongeza ushuhuda wa mwigizaji huyo kabla ya kuanza kumwombea na kumzawadi kwa vyakula kochokocho na pesa.

"Nasikia Mungu akiniambia nikupandie mbegu. Nakubariki na pesa za tambiko. Nitakubariki na vitu zangu za kukula ziko hapa ofisini na pia nikubariki na elfu saba. Wakati huo mwingine wewe ndio utakuja kutuombea," Kanyari alisema.

Mwigizaji huyo alijawa na furaha kupitiliza wakati alipokuwa anapokea vyakula hivyo na bidhaa zingine kemkem.

Baada ya kumkabidhi bidhaa hizo Kanyari aliwekelea mkono wake kwenye utosi wa Omosh na kuanzisha maombi ambayo yaliishia kwa mwigizaji kuanguka chini kwa mgongo.