"Nakutakia maisha mabaya!" Mejja alaaniwa na aliyekuwa mpenzi wake

Muhtasari

•Wairimu alimtakia baba huyo wa mtoto wake kheri za siku ya kuzaliwa ila akaendelea kumtakia maisha mabaya huku akimshtumu kwa kuwa na maadili maovu.

•Hapo awali Wairimu aliwahi kudai kuwa mwanamuziki huyo alimsababishia masaibu mengi katika kipindi cha mahusiano yao.

Mejja na aliyekuwa mpenzi wake Milly Wairimu
Mejja na aliyekuwa mpenzi wake Milly Wairimu
Image: HISANI

Staa wa genge Mejja aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Jumatatu, Mei 23.

Mejja ambaye ametesa kweli kwenye tasnia ya muziki ya Kenya kwa zaidi ya mwongo mmoja alitimiza miaka 36. Mashibiki wake wengi walitumia mitandao ya kijamii kumsherehekea na kumtakia kheri za siku ya kuzaliwa.

Hata hivyo, ujumbe ulionata macho na hisia za  wengi  ni ule wa aliyekuwa mpenzi wake Milly Wairimu ambaye alionekana kama kwamba alikuwa anamlaani mwanamuziki huyo mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake. 

Wairimu alimtakia baba huyo wa mtoto wake kheri za siku ya kuzaliwa ila akaendelea kumtakia maisha mabaya huku akimshtumu kwa kuwa na maadili maovu.

"Heri ya siku ya kuzaliwa. Sikutakii chochote ila maisha mabaya. Ninamaanisha kwamba unapaswa kulipa kwa njia zako mbaya. Jibambe," Wairimu alimwambia Mejja kupitia Instagram.

Ujumbe huo uliashiria kuwa mwanadada huyo bado ana hasira nyingi na Mejja licha ya kuwa mahusiano yao yaligonga ukuta.

Hapo awali Wairimu aliwahi kudai kuwa mwanamuziki huyo alimsababishia masaibu mengi katika kipindi cha mahusiano yao.

"Mazee najua mnapenda huyu msee lakini manze kenye alinipitishia, sidhani kuna binadamu yeyote anayastahili! Siku moja nitazungumza kuhusu hadithi yangu. Kwa sasa napendwa vizuri, niite Mrs B," Wairimu alisema kupitia Instagram.

Mejja alisusia kujibu madai hayo huku akiweka wazi kuwa hayupo tayari kuzungushana na mama huyo wa mtoto wake.

Mejja ni miongoni mwa wasanii ambao wameweza kudumu na kukabiliana na mabadiliko kwenye tasnia ya muziki ya Kenya kwa muda mrefu. Siku za hivi majuzi amekuwa akiimba mtindo mpya wa gengetone.