Harmonize karudiana na Kajala?- Amshukuru mkewe kwa kumchochea kufanya mazoezi

Muhtasari

•Harmonize amesema mpenzi wake wa zamani Frida Kajala Masanja ndiye aliyemchochea kufanya mazoezi zaidi kwenye Gym.

•Siku za hivi majuzi kumekuwa na uvumi kuwa Kajala hatimaye amekubali kumrudia mwanamuziki huyo kufuatia bidii kubwa aliyotia katika kuomba msamaha.

Harmonize na Kajala Masanja
Harmonize na Kajala Masanja
Image: HISANI

Staa wa Bongo Harmonize amesema mpenzi wake wa zamani Frida Kajala Masanja ndiye aliyemchochea kufanya mazoezi zaidi kwenye Gym.

Konde Boy na Kajala ni miongoni mwa wasanii mashuhuri wanaojulikana kupenda kutembelea vyumba vya mazoezi kujenga misuli.

Harmonize amemshukuru mpenzi huyo wake wa zamani kwa kumpatia motisha na kusema anasubiri sana waweze kufanya mazoezi pamoja.

"Asante kwa Motisha mke. Dakika 23 kila siku na nahisi kama sio kitu. Umenifanya kuwa mtu wa msaada na mvulana mzuri tena. Siwezi kusubiri kufanya mazoezi pamoja nawe," Harmonize aliandika chini ya video yake akifanya mazoezi ambayo alipakia Instagram.

Siku za hivi majuzi kumekuwa na uvumi kuwa Kajala hatimaye amekubali kumrudia mwanamuziki huyo kufuatia bidii kubwa aliyotia katika kuomba msamaha.

Hata hivyo hakuna yeyote kati ya wasanii hao wawili ambaye amejitokeza kuthibitisha kuwa wamerudiana. Hivi majuzi Kajala alim-unblock mpenzi huyo wake wa zamani kwenye mtandao wa Instagram.

Akaunti ya Kajala sasa inaweza kuonekana miongoni mwa watu Konde Boy anafuata kwenye Insagram. Hiyo ina maana kuwa Harmonize sasa anaweza kufuatilia chapisho zote za mpenzi huyo wake wa zamani na hata kuchapisha maoni yake chini yake.

Kajala mwenyewe hata hivyo hamfuatilii Harmonize kwenye Instagram labda kwa sababu zake binafsi.

Haya yanajiri takriban mwezi moja unusu baada ya Harmonize kutoa ombi kwa muigizaji huyo kuacha kumfungia kwenye Instagram

Harmonize alitoa ombi hilo mapema mwezi Aprili baada ya kumnunulia muigizaji huyo mkufu wa dhahabu kwa Tsh. 5M.

"Ni tamu sana kutumia pesa zako kwa mtu ambaye unapenda sana. Wa kupeleka sasa!! Milioni 5 kwa pambo la dhahabu.," Harmonize aliandika kwenye Instastori.

Katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja ambacho kimepita Harmonize amekuwa akijaribu njia nyingi za kumuomba msamaha Kajala na kumsihi warudiane. Miongoni mwa mambo ambayo amefanyia mpenzi huyo wake wa zamani ni kumnunulia magari mawili aina ya Range Rover, kuweka bango barabarani, kuomba msamaha hadharani kati ya mambo mengine.