Mulamwah hatimaye akutana na binti yake baada ya miezi 6

Muhtasari

•Mulamwah alipakia picha inayoonyesha akiwa amemshika mtoto huyo wake na muigizaji Carol Muthoni.

•Muthoni alimuomba Mulamwah apige hatua ya kuenda kumuona mtoto wao huku akisisitiza kuwa hana kinyongo chochote dhidi yake.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji Mulamwah hatimaye ameweza kumuona bintiye mwenye umri wa miezi 8 kwa mara ya kwanza ndani ya miezi 6.

Alhamisi msanii huyo kutoka Kitale alipakia picha inayoonyesha akiwa amemshika mtoto huyo wake na muigizaji Carol Muthoni.

"Mimi mdogo.. tumetulia @keilah_oyando," Mulamwah aliandika chini ya picha hiyo ambayo alipakia Instagram.

Hii huenda ni mara ya kwanza mwaka huu kwa mchekeshaji kumuona binti yake kulingana na madai ambayo amekuwa akizua hapo awali.

Mwezi uliopita Mulamwah alidai kuwa miezi mitano ilikuwa imepita tangu mara yake ya mwisho kumuona binti yake.

Akishirikisha wafuasi wake katika kipindi cha maswali na majibu (Q&A) kwenye Instagram, Mulamwah alisema uhusiano mbaya kati yake na mzazi mwenzake ulikuwa unachangia ugumu wa malezi ya pamoja.

"Nimeblockiwa kila mahali, wazazi wetu wamekasirikiana, mambo yameharibika. Familia yangu haijawahi kukutana na mtoto huyo tangu kuzaliwa kwake isipokuwa baba yangu ambaye alifunga safari kutoka Kitale kuja Nairobi. Tulikuwa tumepangia binti yangu karamu nyumbani, kila mtu alihudhuria lakini hakuja na K," Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni muuguzi alidai hajawahi kupata nafasi ya kuwepo katika maisha ya binti yake.

Carol Muthoni alipotembelea studio zetu mwezi Februari alisema mara ya mwisho kwa Mulamwah kumuona mtoto wao ni akiwa na umri wa miezi miwili tu.

Muthoni alimuomba mpenziwe huyo wa zamani apige hatua ya kuenda kumuona mtoto wao huku akisisitiza kuwa hana kinyongo chochote dhidi yake.

"Tenga wakati uje uone mtoto wako, anaendelea vizuri. Ningependa uje uwe katika maisha yake. Uko karibu kila wakati. Hatukukatazi kuja kuona mtoto. Unajua kwangu ni kwako pia. Usijihisi umetengwa," Muthoni alisema.

Siku za hivi majuzi kumekuwa na uvumi mwingi kuwa huenda wawili hao wapo pamoja licha ya drama ambazo zimetokea kati yao kwa muda mrefu.

Wazazi wenza hao wawili wameonekana pamoja mara kadhaa siku za hivi majuzi.