"Enda utafute kazi!" Ex wa Stivo Simple Boy amkataa jamaa anayedai kuchumbiana naye

Muhtasari

•Jamaa aliyejitambulisha kama Eddy alionekana jijini Nairobi akiwa ameshika bango lenye ujumbe mtamu kwa kidosho huyo mwenye umri wa miaka 20.

•Vishy amekosoa hatua ya Eddy kusimama nje ya jengo la Archives na kuweka wazi kwamba hayupo tayari kujitosa kwenye mahusiano naye.

Pritty Vishy na Eddy
Pritty Vishy na Eddy
Image: HISANI

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amekataa ombi la jamaa anayetamani kuchumbiana naye.

Wiki jana  jamaa aliyejitambulisha kama Eddy alionekana jijini Nairobi akiwa ameshika bango lenye ujumbe mtamu kwa kidosho huyo mwenye umri wa miaka 20.

"Nimechoka kukusubiri Pritty Vishy. nakupenda sana mpenzi. Njoo uchukue moyo wangu. Eddy anakupenda," Bango la Eddy lilisoma.

Akizungumza na Nicholas Kioko kwa simu, Pritty Vishy alisema jamaa huyo ni mtafuta kiki tu aliyekosa mwelekeo.

Kipusa huyo alikosoa hatua ya Eddy kusimama nje ya jengo la Archives na kuweka wazi kwamba hayupo tayari kujitosa kwenye mahusiano naye.

"Mimi sipo tayari. Kama hana kazi aende atafute kazi... Enda utafute kazi, fanya kazi, wachana ni vitu mingi. Ata heri angenitumia ujumbe... Sina nia naye. Simpendi," Vishy alisema.

Eddy hata hivyo alitangaza kuwa hatakata tamaa huku akieleza kwamba ana imani kubwa kuwa hatimaye Vishy atashusha moyo wake 

Alisema kuwa anavutiwa sana na urembo wa mpenzi huyo wa zamani wa Simple Boy na yupo tayari kutafuta mahari ya Ksh2M anayodai. 

"Ni msichana mrembo. Mimi nampenda. Maumbile yake hunimaliza. Sura na sauti ndiyo udhaifu wangu kwake," Alisema.

Aliongeza, "Saa hii kazi, nimefutwa. Milioni mbili sina. 2M sidhani inaweza kuwa tatizo, nitaitafuta bora tuelewane."

Jamaa huyo anadai kuwa moyo wake ulianza kumpenda Vishy pindi baada ya mahusiano yake na Stivo Simple Boy kufichuka hadharani.

"Nipe nafasi tu utajua mimi ni malaika nimetumwa kwa ajili yako," Eddy alimsihi Vishy.