Rayvanny afichua gharama kubwa ya tukio la nyumba inayoteketea kwenye video ya wimbo wake

Muhtasari

•Rayvanny amesisitiza kuwa tukio la moto kwenye video hiyo ambayo aliachia mapema wiki hii sio la kutengenezwa ila ni tukio halisi.

•Baadhi ya wanamitandao wametilia shaka tukio hilo huku wengine wakishangazwa na hatua ya mwanamuziki huyo.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Staa wa Bongo Rayvanny amefichua kuwa sehemu ya video ya wimbo wake na Zuchu  'I Miss You' inayoonyesha nyumba inayochomeka ilimgharimu Tsh 15M. (Ksh 750, 000).

Rayvanny amesisitiza kuwa tukio la moto kwenye video hiyo ambayo aliachia mapema wiki hii sio la kutengenezwa ila ni tukio halisi kabisa.

"Milioni 15 kwa nyumba kuchomeka," Rayvanny alifichua kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo wa WCB alifichua kuwa video hiyo haikutengenezwa kwa urahisi na ilichukua miezi mitatu kukamilika.

Alieleza kuwa ilikuwa ndoto yake kuweka uhalisia katika video hiyo na ndio maana akaamua kujenga nyumba na kuichoma moto.

"Nilisema nitajenga nyumba na nitaichoma moto. Timu yangu iliniona sio mzima na hatimaye tuliifanya. Pesa nyingi zaidi na tukaichoma yote. Kuweka uhalisia tu," Alisema Rayvanny.

Kulingana na staa huyo wa Bongo, hii ni moja wapo ya video ambazo ametumia pesa nyingi kwalo kutokana naubunifu uliotumika.

Jambo hili limezua mdahalo mkubwa na hisia tofauti miongoni mwa mashabiki na wafuasi wa muziki wa Bongo.

Baadhi ya wanamitandao wametilia shaka tukio hilo huku wengine wakishangazwa na hatua ya mwanamuziki huyo.

Vifaa vilivyotumika kujenga nyumba hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo wengi wamekuwa na maswali mengi kuhusu huku baadhi ya tetesi zikidai kuwa ilijengwa kwa kutumia katoni.

Hata hivyo Rayvanny mwenyewe bado  hajajitokeza kueleza ukweli kuhusu kilichotumika kujenga nyumba hiyo.