Jalang'o awasaka wafanyikazi wake ambao anadai walitoweka baada ya kuiba pesa

Muhtasari

•Jalang'o  ameahidi zawadi ya Ksh 100, 000 kwa yeyote ambaye atasaidia katika kukamatwa kwa wafanyikazi wake wawili ambao amewashtumu kwa kuiba.

•Jalang'o ameomba yeyote atakayewaona wafanyikazi hao wake kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha karibu

Image: INSTAGRAM// JALANG'O

Mgombea kiti cha ubunge cha Lang'ata Felix Odiwour almaarufu Jalang'o  ameahidi zawadi ya Ksh 100, 000 kwa yeyote ambaye atasaidia katika kukamatwa kwa wafanyikazi wake wawili ambao amewashtumu kwa kuiba.

Jalang'o amewashtumu Morrison Litiema na Eli Khumundu kwa kuiba pesa ambazo zilikuwa zimeachwa ndani ya gari ambalo walikuwa wanaosha Jumamosi asubuhi.

Mtangazaji huyo wa zamani amedai kuwa wawili hao ambao wamekuwa wakihudumu kama watunza nyumba na bustani wake walitoweka na familia zao baada ya kuiba pesa hizo na hata kuzima simu zao.

"Eli na Litiema wanakimbia, leo asubuhi waliiba pesa kwenye gari walilokuwa wakiosha nyumbani, simu zao zimezima na wanakimbia na familia zao," Jalang'o alisema kupitia Instagram.

Mchekeshaji huyo ambaye anatazamia kuingia bungeni kwa mara ya kwanza ameomba yeyote atakayewaona wafanyikazi hao wake kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha karibu.

"Ukiwaona tafadhali wasiliana 0722915337 au toa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu nawe Zawadi ya 100k kwa taarifa yoyote itakayopelekea kukamatwa kwao," Alisema.

Jalang'o hata hivyo hakubainisha kiasi cha pesa ambazo ziliibiwa wala ikiwa zilikuwa zake ama za mtu mwingine.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha za wafanyikazi kazi hao wake ambao wamekuwa wakimfanyia kazi kwa muda mrefu.

Mchekeshaji huyo aligura kazi ya utangazaji takriban miezi minne iliyopita ili kuangazia kampeni zake .

Anawania ubunge wa Lang'ata kwa tikiti ya chama  ODM kinachoongozwa na mgombea rais Raila Odinga.