"Sitaki kujitia aibu!" Wema Sepetu azungumzia suala la kujitosa kwenye kuimba

Muhtasari

•Wema Sepetu ameweka wazi kuwa yeye  hajabarikiwa na kipaji cha kutengeneza muziki na kuuimba.

•Wema alifichua kuwa amewahi kuingiza sauti yake kwenye nyimbo kadhaa za aliyekuwa mpenzi wake, Diamond

Image: INSTAGRAM// WEMA SEPETU

Muigizaji maarufu kutoka Bongo Wema Sepetu ameweka wazi kuwa hana mpango wa kujitosa kwenye sanaa ya muziki.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akizinduliwa kama balozi mpya wa Kodtec, Wema alisema kuwa hajabarikiwa na kipaji cha kutengeneza muziki na kuuimba.

Mpenzi huyo wa zamani wa mwanamuziki Diamond Platnumz hata hivyo alibainisha kuwa ana uwezo wa kuingiza sauti yake kwenye nyimbo za wasanii wengi.

"Mimi huwa napenda kuingiza zile sauti za nyuma. Kuimba siwezi, sitaki kujitia aibu. Kama wasanii wanapenda ssauti zile za nyuma, mimi niko vizuri Hamna wimbo wowote wa Wema unakuja, sitegemei kuingia kwenye kuimba kwa kweli. Mtanicheka nikianza kuimba, siko tayari," Wema alisema.

Wema alifichua kuwa amewahi kuingiza sauti yake kwenye nyimbo kadhaa za aliyekuwa mpenzi wake, Diamond. Alifichua kuwa 'Lala Salama' na 'Chanda Chema' ni baadhi ya nyimbo za Diamond ambao sauti yake ipo ndani.

"Mimi huwa na sauti nzuri sana ya nyuma. Hata nyimbo za Naseeb nimewahi kuingiza sauti sana," Alisema.

Aidha mshindi huyo wa  Miss Tanzania 2006 alidokeza kuwa huenda akafanya mradi na Diamond hivi karibuni.

 Wema alifichua kwamba kwanza anakusudia kumualika Diamond katika shoo yake ya Cook with Wema na tayari ametoa wito kwa bosi huyo wa WCB akubali mwaliko wake wakati huo utakapofika.

"Bwana Simba nitakapokuja kukuomba ushiriki katika kipindi changu basi naomba unipokee kwa mikono miwili. Nina imani tutafanya kipindi ambacho kitakuwa kizuri sana ambacho hakijawahi kutokea tangu  Cook with Wema ilipoanza," Wema alisema.

Alisema kwamba yeye yupo tayari kabisa kuwa na kikao na bosi huyo wa WCB huku akiweka wazi kwamba hatamlazimisha kushiriki.

"Akinikatalia nitamshtaki kwa wananchi ili mnisaidie kumuomba. Kuhusu mradi wetu wa Temptations kwa sababu hapa katikati kumetokea vitu vingi, sijui, mimi niko tayari kabisa kufanya kazi na mwenzangu. Sasa inategemea na yeye, inahitaji pande zote ziingiane na ziwe tayari. Mimi mwenyewe niko tayari , kama mwenzangu pia yupo tayari mbona isifanyike. Lengo ni kutumbuiza watu tu" Alisema.