Dalili zinazoashiria kuwa Harmonize na Kajala tayari wamerudiana

Muhtasari

•Dalili kuwa huenda tayari wametupa mzozo wao kwenye kaburi la sahau na kukubali kurudiana zilianza kujitokeza wiki chache zilizopita.

•Jumatatu Harmonize alipakia picha ya Kajala akiwa ndani ya nyumba ambayo inaaminika kuwa ni yake. 

Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Image: HISANI

Hisia kwamba mwanamuziki Harmonize na muigizaji Frida Kajala hatimaye wamerudiana imeendelea kutanda kote Afrika Mashariki.

Hii ni kutokana na matukio ya hivi majuzi ya wasanii hao wawili wa Tanzania haswa kwenye mitandao ya kijamii.

Dalili kwamba huenda tayari wametupa mzozo wao kwenye kaburi la sahau na kukubali kurudiana zilianza kujitokeza wiki chache zilizopita wakati Kajala aliondoa block ambayo alikuwa amemwekea Harmonize kwenye Instagram.

Harmonize pia alianza kumtambua Kajala kama 'mke' wake katika chapisho zake za Instagram ambazo zilimlenga.

Takriban wiki mbili zilizopita Harmonize aliandika ujumbe wa pongezi kwa Kajala akidai kuwa alimpatia  motisha wa kufanya mazoezi.

"Asante kwa Motisha mke. Dakika 23 kila siku na nahisi kama sio kitu. Umenifanya kuwa mtu wa msaada na mvulana mzuri tena. Siwezi kusubiri kufanya mazoezi pamoja nawe," Harmonize aliandika chini ya video yake akifanya mazoezi ambayo alipakia Instagram.

Mwanamuziki huyo aliendelea kumtaja Kajala kama mke wake katika chapisho zake nyingi kwenye mtandao huo.

Jumapili hatimaye Kajala alijibu chapisho moja la bosi huyo wa Konde Music Worldwide, jambo ambalo liliwasisimua sana mashabiki.

Katika chapisho hilo Harmonize alikuwa anampongeza Kajala kwa kusimama naye katika hali zote licha ya mabaya aliyomtendea. Pia alithibitisha kuwa ni kweli alichorwa tattoo ya muigizaji huyo na binti yake Paula kwenye mguu wake wa kulia.

"Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa nilikosea familia yangu. Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa ni familia yangu. Pia hakuna ambacho kitabadilisha kuwa najivunia familia yangu Mguu Wangu wa kulia utasema Sorry mpaka Siku Yangu Ya Mwisho... Nakupenda sana mke wangu Frida Kajala," Alisema.

Ni wazi kuwa Kajala ambaye ndiye alikuwa mlengwa aliweza kuona ujumbe huo, akausoma na kuupenda.

"🙏🏽🙏🏽🙏🏽❤️" Kajala alijibu.

Jumatatu Harmonize alipakia picha ya Kajala akiwa ndani ya nyumba ambayo inaaminika kuwa ni yake. 

Staa huyo wa Bongo pia alipakia video nyingine ikionyesha kabati yake ya nguo na kusema kuwa imekuwa muda mrefu tangu ilipopangwa vizuri hivyo mara ya mwisho.

"Sikumbuki mara ya mwisho kuona nguo zangu zikiwa zimepangwa vizuri hivi. Mapenzi yamenibadilisha kabisa, mimi n mwanaume mpya. Asante mpenzi," Harmonize alisema kuhusu video hiyo, maneno ambayo yanaonekana kumzungumzia Kajala.

Meneja wa mwanamuziki huyo, Choppa TZ pia alifichua kuwa Kajala sasa ndiye bosi wa timu ya mameneja wake.

Choppa alimkaribisha muigizaji huyo katika timu yao na kusema kuwa anafurahia sana kufanya kazi naye.

"Niruhusu nimkaribishe katika timu ya usimamizi mkurugenzi na meneja mpya Frida Kajala. Nimefurahi kufanya kazi na wewe shem," Choppa alisema.

Matukio haya ni dalili kuwa Kajala tayari amekubali msamaha wa mwanamuziki huyo na hata kukubali kurejesha mahusiano. Hata hivyo bado hakuna yeyote kati yao aliyejitokeza wazi kutangaza hatua hiyo.