Kawira wa Papa Shirandula afunguka sababu za kugura ndoa yake ya miaka sita

Muhtasari

•Kawira alisema aligura ndoa yake Juni 2020 baada ya kuwa ameishi na mumewe kwa takriban miaka sita.

•Kawira alisema kabla ya kufikia hatua ya kutengana, yeye na mumewe walikuwa wamejaribu mbinu zote za kutatua tofauti zao.

Muigizaji Joy Karambu almaarufu Kawira
Muigizaji Joy Karambu almaarufu Kawira
Image: HISANI

Muigizaji Joy Karambu almaarufu Kawira amefichua kuwa amekuwa single kwa kipindi cha miaka miwili ambacho kimepita.

Akiwa kwenye mahojiano na Kamuhunjia, Kawira alisema aligura ndoa yake Juni 2020 baada ya kuwa ameishi na mumewe kwa miaka sita.

Muigizaji huyo wa zamani wa Papa Shirandula aliweka wazi kuwa yeye ndiye aliyeamua kuacha ndoa yake baada ya kutoridhishwa na jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea.

"Wakati ambapo nilikuwa najua baadhi ya mambo ambayo najua sasa hivi ilikuwa ni kuchelewa sana. Nilikuwa tayari kwenye ndoa. Tulichumbiana miaka miwili. Kama hutaki kitu kijulikane mtu anaweza kuficha muda mrefu. Sisi tulikuwa watu wa kanisa lakini kuna mambo mengi ambayo hatukuwa tukijua. Baadae tuliona hatuwezi kuendana," Kawira alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alisema miaka sita ya ndoa yake haikufikia matarajio yake na ndiposa akaamua kutoka.

Alieleza kuwa kabla ya kufikia hatua ya kutengana, yeye na mumewe walikuwa wamejaribu mbinu zote za kutatua tofauti zao.

"Tulijaribu kusuluhisha lakini hatukukusudiwa kuwa pamoja. Tulijaribu. Kila mtu alitaka ifanye kazi lakini haikukusudiwa kuwa," Alisema.

Muigizaji huyo aliweka wazi kuwa mawasiliano kati yake na aliyekuwa mumewe yalifika kikomo baada yao kutengana.

Aidha alifichua kuwa ingawa amepiga hatua kubwa za kusonga mbele na maisha yake, bado hajafanikiwa kuponya moyo wake kikamilifu.

"Sipo kwenye mahusiano hayo tena. Tulitengana. Niliondoka," Kawira alisema.

Pia alibainisha kuwa hatarajii kuwa itawahi kufikia wakati arudiane na mume huyo wake wa zamani.