"Haya pia yatapita" Dacha amfariji Akuku Danger anapoadhimsha siku ya kuzaliwa hospitalini

Muhtasari

•Mchekeshaji Akuku Danger anaendelea kupokea matibabu katika hospitali baada ya kulazwa mapema wiki hii.

•Akisherehekea siku ya kuzaliwa ya mchekeshaji huyo, Dacha alimtakia mpenzi huyo wake afueni ya haraka.

Image: INSTAGRAM// AKUKU DANGER

Mchekeshaji wa Churchill Show Mannerson Oduor almaarufu Akuku Danger leo hii anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa kawaida, inapaswa kuwa siku ya furaha kwa msanii huyo ila kwa bahati mbaya hatoweza kuisherehekea jinsi ifaavyo.

Hii ni kwa sababu anaendelea kupokea matibabu katika hospitali baada ya kulazwa mapema wiki hii. Muigizaji Sandra Dacha ndiye aliyetangaza habari kuhusu kulazwa kwa Akuku Danger.

"Akuku Danger amelazwa tena," Dacha alitangaza Jumanne kupitia Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya chumba cha HDU katika hospitali ambayo hakufichua jina.  Dacha hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu ugonjwa wa Akuku.

Akisherehekea siku ya kuzaliwa ya mchekeshaji huyo, Dacha alimtakia mpenzi huyo wake afueni ya haraka.

"Kheri za siku ya kuzaliwa Akuku Danger na afueni ya haraka. Haya pia yatapita," Alisema.

Akuku alilazwa hospitalini mapema wiki hii, takriban miezi mitano baada ya kuruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kuwa amelazwa kwa kipindi kirefu.

Mchekeshaji huyo alikuwa ameshambuliwa na ugonjwa wa pneumonia ambao ulimsababishia matatizo ya kupumua. Pia alikuwa amekumbwa na matatizo ya moyo.

Hapo awali mchekeshaji huyo aliwahi kufichua kuwa  alizaliwa na ugonjwa wa Anemia ya Seli Mundu (Sickle-Cell anemia). Alifichua kwamba madaktari waliwahi kubashiri kuwa angeaga akiwa na miaka 15.

"Nilipokuwa na umri wa miaka 15, daktari aliniambia na mamangu tuende nyumbani nisubiri kufa. Akamwambia wamefanya kila wawezalo. Mama yangu alikuwa mtu wa dini hivyo aliendelea kuomba. Nilimwambia mama anipeleke nyumbani na nikaomba tumpigie simu mchungaji aje aniombee, nilikuwa na maumivu makali sana lakini sikuwa amini kuwa nitakufa," Akuku alisema.

Akuku alisema huwa anakumbwa na uchungu mwingi kila mara ugonjwa huo unaposhambulia tena.  Mojawapo ya dalili ambazo humkumba ni kubadilika kwa rangi ya macho.