Baadhi ya wasanii wa Tanzania ambao wamewahi kutoka kimapenzi na vipusa wa Kenya

Muhtasari

•Wakenya wengi wamewahi kuolewa ama kuoa kutoka Tanzania na vile vile kuna Watanzania wengi ambao wamewahi kutoa mke/mume Kenya

Image: INSTAGRAM// DIAMOND, ALIKIBA, JUX

Kwa miaka mingi Kenya na Tanzania zimebadilishana vitu vingi kutokana na ujirani na uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Baadhi ya vitu ambavyo nchi hizo mbili za Afrika Mashariki zimebadilishana ni pamoja na tamaduni, madini, mazao ya shamba, bidhaa za viwandani na hata watu.

Tukisema mataifa hayo yamebadilishana watu inamaanisha kuna wazaliwa wengi wa Kenya ambao wamehamia Tanzania na kinyume chake.

Baadhi ya sababu ambazo zimewafanya watu kuhama kati ya nchi hizo ni pamoja na ndoa, kazi, masomo na zinginezo.

Wakenya wengi wamewahi kuolewa ama kuoa kutoka Tanzania na vile vile kuna Watanzania wengi ambao wamewahi kutoa mke/mume Kenya.

Katika makala haya tutaangazia baadhi ya wasanii mashuhuri wa Tanzania ambao wamewahi kuchumbia au kuoa wanadada wa Kenya.

1. Diamond Platnumz

Bosi huyo wa WCB aliwahi kuwa kwenye mahusiano na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kifupi kati ya 2019-2020.

Katika kipindi cha mahusiano yao wasanii hao wawili walipata mtoto mmoja pamoja anayejulikana kama Naseeb Junior.

2. Alikiba

Staa wa Bongo Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba amekuwa kwa ndoa na binti kutoka Mombasa, Amina Khalef.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2018 na tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.

Mapema mwaka huu tetesi zilichimbuka kuwa Bi Amina aliwasilisha ombi la talaka katika mahakama ya Kadhi. Hata hivyo haijathibitishwa ikiwa wawili hao wako pamoja bado ama walitalikiana.

3. Ben Pol

Mwanamuziki Ben Pol alikuwa kwenye ndoa na mfanyibiashara wa Kenya Anerlisa Muigai kwa kipindi kifupi.

Wawili hao walifunga pingu za maisha mwaka wa 2020 ila wakatengana takriban mwaka mmoja baadae.

4. AY

Staa wa Bongo Ambwene Allen Yessayah almaarufu AY na malkia wa muziki wa Kenya Amani walikuwa kwa ndoa kwa takriban miaka miwili.

Wasanii hao wawili walifunga pingu za maisha mwaka wa 2005 ila ndoa yao ikagonga ukuta mwaka wa 2007.

5. Dkt Jimmy Chansa

Daktari mashuhuri Jimmy Chansa alimchumbia mwanasoshalaiti wa Kenya Vera Sidika kwa kipindi kifupi takriban miaka mitatu iliyopita.

6. Jux

Staa wa Bongo R&B Juma Jux anadaiwa kuwa kwenye mahusiano na mwanasoshalaiti wa Kenya Huddah Monroe.

Wawili hao wameonekana wakikumbatiana na kupigana busu hadharani mara kadhaa katika siku za hivi majuzi.

Hata hivyo wamekuwa wakitupilia mbali madai ya mahusiano huku wakieleza kuwa uhusiano wao ni wa kirafiki tu.