Mjukuu wa Kibaki afunguka bado anamuomboleza babu yake miezi miwili baada ya kifo chake

Muhtasari

•Sean Andrew amefichua kuwa ukimya wake kwenye mitandao ya kijamii ulichangiwa zaidi na hali ya kuwa bado anaomboleza.

•Amepongeza upendo mkubwa ambao wanamitandao wa Kenya walimuonyesha wakati alipompoteza babu yake.

Sean Andr3w
Image: Instagram

Takriban miezi miwili baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya Emilio Mwai Kibaki, mjukuu wake Sean Andrew bado hajaweza kukabiliana na majonzi.

Sean Andrew ni miongoni mwa watu maarufu zaidi kutoka familia ya rais huyo wa zamani. Yeye ni mwanawe Jimmy Kibaki, mtoto wa pili wa hayati Kibaki. 

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa shoo halisi ya Betty Kyalo, mwanamitindo huyo alifichua kuwa ukimya wake kwenye mitandao ya kijamii ulichangiwa zaidi na hali ya kuwa bado anaomboleza.

"Mimi naomboleza. Ninajaribu kuwa na heshima kwa njia bora niwezavyo," Andrew alisema.

Andrew ana ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na kwa muda mrefu amekuwa akitumia kurasa zake kuonyesha mitindo yake na kutangamana na Wakenya. Hata hivyo hajakuwa akionekana sana kmitandaoni tangu babu yake alipoaga mnamo Aprili 22 mwaka huu.

Mwanamitindo huyo amepongeza upendo mkubwa ambao wanamitandao wa Kenya walimuonyesha wakati alipompoteza babu yake.

"Sisi Wakenya tunashirikiana sana. Nilifurahia sana kupokea upendo mkubwa kutoka kwa Wakenya wakati wa kipindi kigumu ambacho tulipitia sote. Nina raha na tuendelee na tamaduni hiyo," Alisema

Andrew pia amedokeza kuwa hana mpango wa kujitosa kwenye ulingo wa siasa kama marehemu babu yake.

Alisema kuwa anaridhika zaidi kutoa mchango wake kwa Wakenya kama raia wa kawaida, jambo ambalo anakusudia kuendelea nalo.

"Sioni haja ya siasa katika maisha yangu. Nadhani naweza kuwasaidia Wakenya zaidi nikiwa kama raia wa kawaida. Mtu yeyote anaweza kuboresha maisha ya Wakenya, sio wanasiasa tu," Alisema.

Mwanamitindo huyo pia aliweka wazi kwamba huwa anapendelea kuweka siri ya  maisha yake ya kibinafsi.